Na Lucy Lyatuu
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Dkt Emmanuel Tutuba amewahakikishia wananchi kuwa sekta ya benki nchini iko imara na wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi Wala mashaka yoyote pale wanapotumia huduma za benki.
Dkt. Tutuba ameyasema hayo mara baada ya kutembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania linaloshiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam -(Sabasaba)
“Amesema kuwa wananchi ambao wanatumia huduma mbalimbali za benki hawapaswi kuwa na wasiwasi wowote kwani sekta hiyo muhimu kwa uchumi imeimarika vya kutosha,” amesema.

Kuhusu ushiriki wa BOT katika maonesho hayo, Gavana Tutuba alisema hatua hiyo imechangia pakubwa katika utoaji wa elimu kwa wananchi.
Gavana Tutuba amebainisha kuwa kupitia banda la BOT, wananchi wanapata elimu kuhusu sera za fedha, jinsi ya kujikinga na ulaghai, matumizi sahihi ya huduma za benki na kidijitali.
Amesema BOT itaendelea kusimamia mfumo wa benki ili uwe imara, salama na uweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Hata hivyo ,BoT imetangaza kiwango kipya cha riba ya robo tatu ya mwaka kuwa asilimia 6.25,hivyo kiwango hicho kitaleta utulivu wa bei nchini.

Ameongeza kuwa maoneaho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ni fursa nzuri kwa BOT kutoa eleimu kwa wananchi kuhusu sera za fedha na huduma za benki
Kuhusu maadhimisho ya miaka 60 ya BOT, amesema taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika kuimarisha utulivu wa uchumi, usimamizi wa sekta ya benki, mifumo ya malipo, elimu ya fedha na upatikanaji wa huduma za kifedha nchini.
Amesema mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi tulivu na mfumo imara wa kifedha unaovutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi

