Na Lucy Ngowi
DODOMA: RAIS Samia Suluhu Hassan ameagiza kusimamiwa kikamilifu utekelezaji wa sera na Mitaala mipya ya elimu, ili ilete matokeo yaliyokusudiwa katika kuimarisha sekta ya elimu.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo Februari mosi, 2025 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la mwaka 2023 iliyofanyika mkoani Dodoma.
Samia ameziagiza Wizara ya Fedha, Wizara ya Mipango na Uwekezaji. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuwezesha kusimamia utekelezaji wa Sera na Mitaala hiyo mipya.

Amesema mabadiliko ya kukua kwa kasi kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( TEHAMA), kunaweza kuwa mchango chanya au hasi kutokana na namna jamii itakavyojipanga.
“Ili kuendana na mabadiliko hayo ni lazima kutumia TEHAMA kutoa elimu kwa urahisi na kuwaandaa vijana wetu kuwa na taaluma na ujuzi wa taaluma zinazoendana na mageuzi ya TEHAMA bila kuathiri maadili ya vijana hao,” amesema.
Pia Rais Samia amesema serikali haina budi kuwa na maandalizi ya kutosha kwa kuinua viwango vya ubora wa elimu, kuwaandaa vijana vizuri zaidi ili wamudu stadi muhimu zitakazowawezesha kuajiriwa na kujiajiri, kuwajengea ujasiri na kuweza kujiamini.
Amesema dhamira ya kufanya mabadiliko katika Sera ni kumuandaa kijana anayejiamini na mwenye nyenzo stahiki za kukabiliana na ushindani wa kikanda na kimataifa ili kutumia utajiri wa rasilimali za nchi, anufaike kiuchumi.

“Sera iliyoboreshwa pia italeta somo la ujasiriamali ambalo litakuwa la lazima kwa kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne ili kumuandaa mwanafunzi kupata misingi ya biashara,” amesema.
Amesema ili mwanafunzi huyo akiamua kujiajiri kwa kutumia stadi alizopata shuleni, aweze kufanya shughuli zake akiwa na maarifa ya biashara na apate manufaa zaidi.