IHNBC Yamtunuku Shahada ya Heshima ya Uzamivu
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHUO cha In His Name Bible College (IHNBC) cha nchini Marekani kimemtunuku Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Utawala na Maendeleo ya Rasilimali Watu, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Suleiman Ikomba.

IHNBC kimemtunuku Ikomba kwa kutambua mchango wake mkubwa katika uongozi na maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Hafla hiyo ya mahafali ya pili ya chuo hicho imefanyika leo Septemba 13, 2025 jijini Dar es Salaam, katika Kanisa la Baptist, Kinondoni B, ambapo jumla ya wahitimu 21 walitunukiwa vyeti vyao katika ngazi mbalimbali za kitaaluma.

Miongoni mwa wahitimu hao, watatu walipata Diploma ya Theolojia, watano walitunukiwa Shahada ya Kwanza, 12 walipokea Shahada za Uzamivu za Heshima, huku mmoja akitunukiwa cheo cha Uprofesa wa Heshima.

IHNBC ni taasisi ya kimataifa ya mafunzo ya Biblia na maendeleo ya uongozi, yenye makao makuu yake nchini Marekani, na inatoa mafunzo na tuzo mbalimbali za heshima kwa watu wanaojitolea katika kuboresha maisha ya jamii kupitia huduma ya kiroho, elimu na uongozi.


