– Dkt. Ikomba Aahidi Kutumikia Taifa Kwa Moyo Wa Uzalendo Na Kujitolea
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: PROFESA mteule Julius Laizer ametunukiwa uprofesa wa heshima na Chuo cha In His Name Bible College (IHNBC) cha Marekani, na kuahidi kutumia heshima hiyo kupambana na changamoto kuu zinazokwamisha maendeleo ya Watanzania ikiwemo ujinga, umaskini na maradhi.

Amesema hayo katika mahafali ya pili ya chuo hicho yaliyofanyika katika Kanisa la Baptist, Kinondoni B jijini Dar es Salaam.
Amesema atatumia ndoto hiyo kupambana na hao maadui watatu.
“Laizer amesema kutunukiwa uprofesa wa heshima ni kutimia kwa ndoto yake ya utotoni.
“Tangu nikiwa na umri wa chini ya miaka nane nilitamani kusoma na kuwa mtu mkubwa. Leo hii, ndoto hiyo imetimia,” amesema Profesa Laizer.
Amesisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya nchi yoyote na kuitaka jamii kuihifadhi kwa nguvu zote.
“Dumisheni amani Tanzania, maana amani ni bora kuliko vitu vyote. Amani ikiwepo, haki hutendeka,” amesema.
Amewahimiza Watanzania kufanya kazi kwa bidii, kuwa wabunifu na kutumia elimu kama silaha ya kupambana na umasikini na ujinga, akiongeza kuwa maendeleo yanahitaji juhudi za pamoja.

Katika mahafali hayo, wahitimu 21 walitunukiwa vyeti mbalimbali, watatu walipewa diploma ya theolojia, watano shahada ya kwanza ya theolojia, 12 walitunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima akiwemo Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Dkt. Suleiman Ikomba,
Na mmoja Julius Laizer alitunukiwa uprofesa wa heshima kwa mwaka wa masomo 2024/2025.
Miongoni mwa waliotunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima yumo Mchungaji Jonathan Mtibona wa Kanisa la EAGT Ilemela, Mwanza, ambaye amesema heshima hiyo ni ishara ya kutambuliwa kwa kazi yake ya utumishi kwa jamii na kanisa.

“Nimeweza kusimamia ujenzi wa makanisa katika mikoa ya Kigoma na Mwanza yenye thamani ya zaidi ya Sh.Bilioni 2. Pia ni mwalimu wa uchumi na mwanzilishi wa shule ya awali kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu inayojulikana kama Maisha Mapya Charity,” amesema Mtibona.
Naye Dkt. Arnold Manase aliyepokea shahada hiyo ya heshima katika fani ya Uongozi na Ushauri Nasaha, amesema shahada hiyo ni kichocheo cha kutumia uwezo wake kikamilifu kwa ajili ya kusaidia jamii.
Rais wa CWT, Dkt. Ikomba, ameeleza kuwa heshima hiyo imempa nguvu na chachu ya kuendelea kulitumikia taifa kwa moyo wa uzalendo na kujitolea.

Chuo cha In His Name Bible College kimeendelea kutoa heshima kwa viongozi wa dini na jamii wanaochangia maendeleo kupitia huduma za kiroho, kijamii na kielimu, ikiwa ni njia ya kuwatambua na kuwahamasisha kuendelea na kazi zao za kiutumishi kwa jamii.