Na Mwandishi Wetu
MFUKo wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), unatarajia kufanya uwekezaji mkubwa katika Jiji la Dodoma kwa kujenga jengo la minara miwili ambalo litachochea ukuaji wa uchumi na utalii katika jiji hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea mradi huo pamoja na zoezi la kupanda miti katika kiwanja namba 3 kitalu F, kilichopo Njedengwa jijini Dodoma.
Mshomba amesema NSSF imeamua kuwekeza katika mradi huo kwa sababu shughuli za uwekezaji ni jambo la msingi na wamekuwa wakiwekeza kwenye maeneo tofauti tofauti .Amesema lengo la kuwekeza ni ili kuhakikisha thamani ya michango ya wanachama haipotei na kupata faida inayoiwezesha Mfuko kulipa mafao kwa wanachama wake.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Moshomba amesema utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza Mei 2025 na utakamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu.
Amesema miongoni mwa faida zinazotarajiwa kupitia mradi huo ni kuchochea utalii wa mikutano, kuvutia wawekezaji na kuongeza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Mradi huo unatarajiwa kugharimu sh bilioni 148.40 kwa gharama za awali za mradi.
Mshomba amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi ambazo amekuwa akizifanya katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, ambapo kwa upande wa NSSF imepata mafanikio makubwa katika miaka ya hivi karibuni kwa kuongeza wanachama na waajiri pamoja na ongezeko la michango na kusababisha thamani ya Mfuko kufikia trilioni 8.5.
“Mafanikio yote hayo yanatokana na juhudi kubwa ambazo Mheshimiwa Rais wetu amezifanya katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, lakini pia juhudi zinazochukuliwa na Bodi ya Wadhamini, Ofisi ya Waziri Mkuu na BoT,” amesema Mshomba.
Amesema Juni 2024, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara ya kikazi katika jiji la Mwanza alitembelea mradi wa uwekezaji wa jengo la hoteli ya nyota tano ambapo alishauri NSSF ikipata mapato mazuri zaidi, uiangalie kuwekeza kwenye maeneo mengine ikiwemo mji wa kiserikali Dodoma, hivyo pamoja na kutekeleza mpango wa NSSF kuwekeza Dodoma kwa mujibu wa miongozo na sera za uwekezaji lakini pia ni utekezaji wa maono na maelekezo ya Rais.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameipongeza NSSF kwa mpango wa utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo mkubwa ambao utachochea ukuaji wa uchumi na utalii katika mkoa huo ambao ndio Makao Makuu ya Nchi, utaleta heshima katika Kanda ya Kati na Taifa kwa ujumla.
Rosemary amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali yenye malengo ya kukuza uchumi pamoja na biashara ya utalii na kuwa mikakati hiyo imeanza kuzaa matunda baada ya RaisDkt. Samia Suluhu Hassan kuifungua nchi pamoja na kuzindua filamu ya ‘The Royal Tour’ ambayo imechangia ongezeko kubwa la watalii.
Amesema ujenzi wa kitega uchumi hicho cha NSSF utakuwa chachu ya kuchochea uchumi.
“Mimi ninaposhuhudia NSSF mnakuja kuwekeza mradi mkubwa wa namna hii nawaona ni waelewa wa haraka sana wa kumuelewa Mhe. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Rosemary.
Amesema mojawapo ya vitu ambavyo Rais anatamani kuviona ni Mkoa wa Dodoma ambao ndio Makao Makuu ya Nchi kuleta mikutano ya kimataifa, hivyo ujenzi wa jengo hilo la kitega uchumi la NSSF linaendana na azma ya Serikali ya awamu ya sita ambayo inaendelea kuufungua mkoa huo pamoja na maeneo mengine nchini.
Rosemary amesema kukamilika kwa hoteli hiyo pamoja na uwanja wa ndege wa Msalato utachochea shughuli za kiuchumi, kufungua fursa mpya za mikutano ya kimataifa jijini humo, kuongeza mnyororo wa thamani pamoja na kuzalisha ajira.
Ametumia fursa hiyo kuipongeza NSSF kwa kupata mafanikio mbalimbali ambapo hivi sasa thamani ya Mfuko imefikia trilioni 8.5 jambo ambalo limechangiwa na kuwepo kwa ongezeko kubwa la wawekezaji, kukua kwa sekta binafsi na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi.
Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja Usimamizi Wa Miradi NSSF Helmes Pantaleo, amesema mradi huo unatarajiwa kujengwa jengo la ghorofa 16 na kuwa umegawanyika sehemu tatu ikiwemo ya ofisi, hoteli na maduka makubwa.
Amesema hoteli hiyo itakuwa na vyumba 120 kikiwemo chenye hadhi ya kulala viongozi wakuu na migahawa mbalimbali.