Na Danson Kaijage
DODOMA: MGOMBEA UQbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Dodoma Mjini, Fatuma Waziri, amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuulizwa maswali na wanachama wa chama chake wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Mpunguzi.
Mmoja wa wajumbe wa CCM kata ya Mpunguzi, Josefu Mhawi, amemuuliza mgombea huyo kuhusu hatma ya wakulima wanapozeeka, ikilinganishwa na wafanyakazi wa kawaida wanaopata mafao yao baada ya kustaafu.

“Tanzania ina watu wawili: wakulima na wafanyakazi. Mfanyakazi anapostaafu analipwa pensheni yake. Mkulima anapozeeka halipwi chochote.
“Je, endapo utachaguliwa kuwa mbunge, utatuteteaje wakulima ili na sisi tulipwe mafao, kwani tumetumia muda wetu kulilisha taifa?” alihoji Mhawi,”amehoji.
Maswali hayo yaliibua mjadala mzito na kumweka mgombea katika hali ya sintofahamu kwa muda, hata akasahau jina la Kata aliyopo.
Kwa upande wake Mjumbe wa CCM katika Kata hiyo, Paulo Lyasweye, amehoji kuhusu namna mgombea huyo atakavyosaidia wananchi kupata mahindi ya msaada na kusema ukweli bungeni kuhusu hali halisi ya mfumuko wa njaa nchini.
“Kumekuwepo na tatizo la njaa kutokana na ukame, lakini viongozi wamekuwa wakilificha suala hili. Wakati mwingine mahindi ya msaada huuuzwa kwa bei ya juu. Je, wewe ukiwa mbunge, utatusaidiaje kupaza sauti bungeni na kupunguza bei ya mahindi ya msaada?” amehoji Lyasweye.
Akijibu maswali hayo, Fatuma amesema iwapo atachaguliwa, atakutana na wananchi kujadiliana jinsi ya kupeleka mapendekezo bungeni ili kuangalia uwezekano wa wakulima kunufaika na mfumo wa mafao.
Kuhusu suala la chakula cha msaada, amesema analiona kama hitaji la msingi linalopaswa kuwekewa mkazo kwa kubadili sera na kuondoa ubabaishaji uliopo sasa.
Wagombea wengine waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ya ubunge walikuwa ni Mhandisi Rashid Mashaka, Pascal Inyasi Chinyele, Samwel Marwa Kisaro, Robert Daniel Mwinje, Rosemary Chabe Jairo na Abdulhabib Jafar Mwanyemba. Kwa pamoja, walitoa ahadi za kupeleka huduma ya maji, kuboresha afya, elimu na ustawi wa wananchi wa Dodoma Mjini.