Na Mwandishi Wetu
GEITA: SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC) limeshiriki katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini, yanayoendelea mkoani Geita, kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kuongeza ukaribu na wateja wake.
Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa NIC, Karimu Meshack, amefanya ziara ya kutembelea mabanda ya taasisi mbalimbali za kifedha, bima na sekta ya madini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kushirikiana kwa karibu na wadau wake.

Miongoni mwa taasisi alizotembelea ni pamoja na Benki ya NMB, Benki ya Equity, Bluecoast, Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Binafsi (NSSF), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Kampuni ya Madini ya FEMA, pamoja na Wakala wa Bima wa HEXAD.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo katika banda la Benki ya NMB, Meshack amesema,

“Tumekuja kuwashukuru kwa kuendelea kutumia huduma za NIC. Pia tunalenga kuimarisha ushirikiano wetu wa kibiashara, kutambua changamoto zilizopo na kuhakikisha tunazitatua kwa wakati.”
Maonesho hayo ambayo hufanyika kila mwaka, yanawakutanisha wadau kutoka sekta ya madini, teknolojia, fedha, na bima, huku kwa mwaka huu yamefunguliwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

NIC imeendelea kutoa huduma na elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Wananchi wanakaribishwa kutembelea banda la NIC lililopo karibu na mabanda ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Chuo cha Teknolojia ya Madini (TTC), kwa ajili ya kupata huduma za bima, ushauri wa kitaalamu na maelezo ya kina kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali za shirika hilo.

