Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amefungua mafunzo ya wataalam kutoka taasisi mbalimbali nchini yanayohusu usanifu, utengenezaji na ufungaji wa mifumo ya Nishati ya Jua na matumizi yake.
Matumizi hayo ni kuchemsha, kupika, kupoza maji pamoja na kukausha mazao kwa kutumia nishati ya Jua.

Akifungua mafunzo hayo Dar es Salaam, Mramba amesema mafunzo kuhusu teknolojia ya nishati ya Jua yanaenda pamoja na vipaumbele vya taifa katika Dira 2050 ambapo Dira hiyo inagusia mikakati ya kuendeleza matumizi ya nishati jadidifu nchini.
“Nishati Jadidifu ikiendelezwa kikamilifu itakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi, itapunguza utegemezi katika nishati isiyosafi ikiwemo kuni na kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati kwa njia ya kisasa zaidi.” Amesema Mramba
Mramba amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kuwa makini na kuzingatia kile kinachofundishwa ili kiweze kuleta tija nchini.
Vilevile, Mramba ameeleza kuwa Tanzania inajivunia ushirikiano wake na mashirika mbalimbali ya Kimataifa katika kuendeleza Sekta ya Nishati ikiwa ni pamoja na kufanikisha mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo wataalam.

Mafunzo hayo ya Nishati ya Jua yanayojulikana kama SOLTRAIN + yameandaliwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Kituo Mahiri cha Matumizi Bora ya Nishati na Nishati Jadidifu (SACREEE) ambacho kipo chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika ( SADC).
Jumla ya washiriki 40 kutoka taasisi mbalimbali wanahudhuria mafunzo hayo ya siku mbili wakiongozwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga.
