Na Lucy Ngowi
GEITA: MKUU wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ameitaka Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kushuka hadi ngazi za chini zaidi, Ili kuhakikisha usalama wa mitaji ya wananchi wanaowekeza kwenye taasisi ndogondogo zisizo rasmi kama Vikundi vya Kuweka na Kukopa (VIKOBA) na Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS).”
Komba ametoa rai hiyo alipotembelea banda la DIB kwenye maonesho ya nane ya Sekta ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.

Amesema wananchi wengi wamekuwa wakipoteza fedha nyingi kutokana na kuwekeza kwenye vikundi visivyosajiliwa au visivyo chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Mara nyingi wananchi wanakuja ofisini kwetu wakilalamika kuwa wamepoteza fedha nyingi, wengine hadi Sh milioni 30, walizowekeza kwenye hisa au vikundi ambavyo si rasmi. Tunaanza kuhangaika kutafuta viongozi wa vikundi hivyo,” amesema.
Amesisitiza kwamba, ni muhimu kwa DIB kushirikiana kwa karibu na Benki Kuu, serikali za mitaa pamoja na taasisi nyingine za kifedha kuhakikisha mifumo ya kifedha ya kijamii kama VICOBA inapata kinga ya kifedha kama ilivyo kwa benki rasmi.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, amesema bodi hiyo inatambua changamoto hizo na iko tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha usalama wa fedha za wananchi.
“Tunaishukuru sana ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ushauri huu. Tunaendelea kushirikiana na Benki Kuu pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha taasisi zote za fedha, kubwa na ndogo, zinakuwa chini ya uangalizi na miongozo bora ya usimamizi,” amesema Mwambande.
Amesema kwa sasa, DIB inalinda amana za hadi Sh Milioni 7.5, na asilimia 99 ya wananchi wenye akaunti katika mabenki wanalindwa iwapo benki itafilisika.
“Lengo letu si tu kuwafidia wananchi pale panapotokea matatizo, bali ni kujenga imani ya wananchi katika mfumo rasmi wa kifedha ili waendelee kuutumia, na hivyo kusaidia kukuza uchumi wa taifa,” aliongeza.
Wito huo wa Mkuu wa Wilaya umetolewa wakati ambapo matumizi ya mifumo ya kifedha isiyo rasmi yanaongezeka, hali inayohitaji usimamizi madhubuti ili kulinda fedha za wananchi na kuimarisha uchumi wa taifa.