Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Ulanga, Salim Hasham, amesema kipaumbele chake cha kwanza ni kuhakikisha barabara ya Ifakara hadi Ulanga inajengwa kwa kiwango cha lami, kama ilivyoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030.
Amesema hayo katika Viwanja vya Bunge leo Novemba 12, 2025 alipozungumza na Waandishi wa Habari.
Amesema jukumu lake kama mbunge ni kusimamia na kuhakikisha ahadi hiyo inatekelezwa, kwani barabara hiyo ni kiunganishi muhimu kwa wananchi wa Ulanga na maeneo jirani.
“Serikali tayari imeanza kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kilombero–Lupilo–Songea, na tunategemea barabara hiyo itasaidia kufungua mkoa wa Morogoro na kuunganisha mikoa ya kusini,” amesema.
Pia amesema mkoa wa Morogoro una mpango wa kujenga barabara nyingine kutoka Mlimba hadi Njombe, lengo likiwa ni kuhakikisha miundombinu ya usafiri inaimarika na kufungua fursa za kiuchumi katika maeneo yote ya mkoa huo.
Katika sekta ya Afya, amesema anapigania ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya ndani ya Jimbo la Ulanga ili kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma bora za afya.
“Hospitali ya sasa ni ya zamani na chakavu. Tunahitaji kituo kipya cha kisasa kitakachokidhi mahitaji ya wananchi wetu,” amesema..
Pia kwenye eneo la Kilimo na Umwagiliaji amesema, jimbo la Ulanga limebahatika kuwa na miradi minne ya skimu za umwagiliaji ambayo tayari imefanyiwa upembuzi yakinifu. Miradi hiyo ipo katika kata za Mpande, Mbuga (Ruaha), Kichangani na Minepa.
Lengo ni kuongeza uzalishaji wa mazao na kuinua kipato cha wakulima wa Ulanga. Katika Sekta ya Madini amesema jimbo hilo lina mradi mkubwa wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya graphite, uliyozinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Madini.
Mradi huo wenye thamani ya Sh. Trilioni 1.3 unatarajiwa kutoa zaidi ya ajira 1,000 za kudumu na zaidi ya ajira 2,000 za muda, jambo litakaloinua uchumi wa eneo hilo.
“Huu ni mradi mkubwa utakaofungua uchumi wa Ulanga. Kupitia CSR, tunatarajia kuona maendeleo makubwa kwenye huduma za jamii, miundombinu na biashara,” amesema.
Akizungumzia Mapato na Maendeleo Endelevu, amesema Kwa sasa, Jimbo hilo linakusanya kati ya Sh. Bilioni 2.5 hadi tatu kwa mwaka, lakini mbunge huyo anatarajia kiwango hicho kitaongezeka maradufu kutokana na uwekezaji mpya unaoendelea.
Amehimiza wananchi wa Ulanga kutambua na kutumia fursa zitakazotokana na miradi ya maendeleo, hasa sekta ya madini, ili kuinua maisha yao na kukuza uchumi wa eneo hilo.
“Tukitumia vizuri fursa hizi, Ulanga itakuwa kitovu cha maendeleo katika mkoa wa Morogoro,” amesema.

