Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR: MAKAMU wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kuelekea uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu 2025, wananchi wanapaswa kupewa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanywa na Serikali zote,
Ili waweze kufanya tathmini na uamuzi wakati wa Uchaguzi wa viongozi wao.

Abdullah ameyasema hayo leo Aprili 3, 2025, alupokuwa akifungua Kikao Kazi cha 20 cha Maofisa Habari wa Serikali kinachofanyika katika ukumbi wa New Aman Complex, Zanzibar.
Abdulla amesema miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Serikali ya Muungano ni ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ili kuimarisha huduma za usafiri wa haraka na kuleta Mapinduzi ya huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo hapa nchini.

Pia amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuimarisha Uwanja cha Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume na vilevile kuanza ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa kimataifa kisiwani Pemba na mingineyo mingi.
Ameeleza kuwa miradi yote hiyo itakapokamilika inakusudiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma, kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo na kupunguza gharama za upatikanaji wa bidhaa kwa wananchi.
Pia kuchochea harakati za kiuchumi hapa nchini.
“Ni wazi kada yenu ina mchango mkubwa kwenye kuhabarisha umma, lakini bado mna kazi kubwa ya kuongeza juhudi ya kuhabarisha Umma kuhusu miradi yote ya maendeleo ili waweze kufanya uamuzi sahihi,” amesema.
Abdullah amewataka maofisa hao waongeze juhudi katika kuhanbarisha umma kwa kutoa taarifa sahihi za miradi mbalimbali ya Serikali.