Na Mwandishi Wetu
MBEYA: KATIBU Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mary Maganga, ametembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu katika maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayoendelea kufanyika kwenye viwanja vya Uhindini, jijini Mbeya.
Maonesho hayo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa kwa mwaka 2025, yakiongozwa na kaulimbiu: ‘Nguvu Kazi ya Vijana kwa Maendeleo Endelevu’.

Maganga amejionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na kujadiliana na vijana kuhusu fursa zilizopo katika maeneo ya ajira, ujasiriamali na ushiriki wa vijana katika maendeleo ya taifa.
Maadhimisho haya yanalenga kuhamasisha ushiriki wa vijana katika shughuli za kijamii na kiuchumi, sambamba na kuonesha mchango wao katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu nchini.



