Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imebaini kuwa baadhi ya watu wasio na sifa za kitaaluma wameanza tena kutekeleza majukumu ya kihabari baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, 2025.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Patrick Kipangula, amesema Bodi inawakumbusha wadau wote kuwa uandishi wa habari ni taaluma rasmi inayosimamiwa na misingi ya kisheria, maadili na weledi wa kitaaluma.
Amesisitiza kuwa mtu yeyote anayejihusisha na shughuli za kihabari bila kuwa na ithibati halali anakiuka masharti ya sheria.
Kipangula ameeleza kuwa makundi yanayotakiwa kuwa na ithibati ni pamoja na wahariri, waandishi wa habari, waandishi huru, wapiga picha za habari, wazalishaji wa vipindi pamoja na watangazaji wa redio na televisheni wanaofanya kazi katika vyombo vya habari.
“Kwa muktadha huo, Bodi inatoa onyo na kuwataka watu wote wanaotekeleza shughuli za kihabari bila kuwa na ithibati kuacha mara moja.
“Kuendelea kufanya hivyo ni kosa kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 50(2)(b) cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229,” amesema.
Ameongeza kuwa Bodi haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu au taasisi yoyote itakayobainika kuajiri au kuruhusu utekelezaji wa kazi za kihabari bila kufuata utaratibu na masharti yaliyowekwa kisheria.
Vilevile, JAB imeutaarifu umma na wadau wa sekta ya habari kuwa katika kipindi cha hivi karibuni itaendesha ukaguzi maalum katika vyombo vya habari na maeneo mbalimbali nchini.
Ukaguzi huo unalenga kujiridhisha kuwa wanaotekeleza majukumu ya kihabari wanakidhi vigezo vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria.
Bodi imetoa wito kwa wote wenye nia ya kufanya kazi za kihabari kuhakikisha wanapata ithibati halali, wanazingatia maadili na weledi wa juu wa taaluma, na kutumia kalamu, sauti na majukwaa yao kuwahudumia wananchi kwa kutoa taarifa sahihi, kukuza uwajibikaji na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.

