Na Lucy Ngowi
WANANCHI wametakiwa wanapokumbana na changamoto wawapo kazini, wafike kwa wakati Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), ili waweze kutatuliwa migogoro yao ya kikazi.
Ofisa Mfawidhi Dar es Salaam wa CMA, Yohana Massawe, amesema hayo wakati akizungumza na Mwandishi wa MFANYAKAZI katika Ofisi za tume hiyo
Massawe amesema wananchi wengi wamekuwa na changamoto ya kutofahamu suala la muda wa kupeleka shauri CMA.
“Mashauri yana muda wa kuwasilishwa na yana muda wa kutatuliwa. Lakini wengi wanachelewa na wanaweza kuwa wanachelewa kwa sababu ambazo sio za msingi lakini mwisho wa siku anaweza kuona hatendewi haki.
“Mnapoondoa labda maombi yake kwa sababu atakapowasilisha maombi ya kusikilizwa nje ya muda lazima aeleze sababu za msingi, mwisho wa siku anaweza kuona hatendewi haki.
“Wengi sasa unakuta hawana sababu za msingi inasababisha maombi yale kuondolewa na shauri lake la msingi kutokuweza kusikilizwa,” amesema.
Amesema elimu inapaswa kuendelea kutolewa kwa wananchi kwamba mtu anapopata changamoto asichelewe akakaa na shida, ama mgogoro wake bila kupata utatuzi, bali afike sehemu husika kwa wakati.
Pia amesema wananchi endapo hawataridhika na matokeo yaliyopatikana, kuna Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, lakini kuna Mahakama ya Rufani pia.