Na Lucy Lyatuu,Dodoma
BODI Ya Bima Ya Amana Tanzania (DIB) imewataka wananchi kutembelea banda la lao lililoko katika maonesho ya Nanenane,jijini Dodoma ili kupata elimu kuhusu mfumo wa Bima ya Amana unaolenga kulinda fedha za wawekaji wa amana katika taasisi za fedha zilizo chini ya mfumo huo.
Mkurugenzi Mkuu wa DIB,Isack Kihwili amesema hayo wakati akizungumza baada ya kutembelea banda hilo lililoko katika maonesho ya Nanenane.
Amesema wananchi wanaoweka fedha katika taasisi zisizo na leseni ya BoT wanajiweka katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa kupata fidia endapo taasisi hizo zitashindwa kuendelea na shughuli zake.
Amesema utaratibu huo umeonyesha umuhimu wake kupitia wateja wa Benki ya FBME ambao walinufaika na mfumo wa fidia uliowekwa na Serikali. Kihwili amewataka pia wawekaji wa amana wa FBME ambao bado wana madai kufika katika banda la DIB kuwasilisha madai yao, ambapo watapatiwa fomu maalumu za kujaza kwa ajili ya kuanza mchakato wa kushughulikiwa kwa madai yao.

Amewataka wananchi kuwa makini katika kuchagua taasisi za fedha wanazoweka fedha zao, akisisitiza umuhimu wa kutumia benki na taasisi zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kulinda haki zao za kupata fidia endapo taasisi hizo zitakumbwa na changamoto za kifedha
Kuhusu mchakato wa ufilisi wa benki ya FBME, Kihwili amesema sheria imeweka utaratibu maalumu wa namna madai yanavyolipwa, ambapo gharama za ufilisi, kodi pale zinapohusika na stahiki za wafanyakazi huzingatiwa kabla ya kushughulikia makundi mengine ya wadai.
“Wenye amana ni miongoni mwa wanaoshughulikiwa katika utaratibu huo, huku kukiwa na makundi mengine ya wadai, wakiwemo waliokuwa wamefungua kesi dhidi ya benki hiyo na kushinda, pamoja na wazabuni,” amesema.
Kihwili amesema wateja wa FBME ambao si wenye amana, wakiwemo wadai waliokwenda mahakamani kudai fedha zao, hawatalipwa katika awamu ya sasa inayolenga kuwalipa wenye amana.
Hata hivyo, amesema DIB inaendelea kufuatilia na kutambua mali za benki hiyo ili kuhakikisha mali zitakazopatikana zinatumika kulipa wadai wengine kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia kiasi kitakachopatikana.
Amesema mara baada ya kukamilika kwa kazi ya kutambua na kupata mali za FBME kwa kiwango kinachowezesha malipo, wadai watatangaziwa na kupewa utaratibu wa malipo kulingana na fedha zitakazopatikana.
“Kwa msingi huo, amewataka wananchi kutumia fursa ya elimu inayotolewa na DIB ili kuelewa haki zao kama wawekaji wa amana na kuhakikisha fedha zao zinawekwa katika taasisi za fedha zilizoidhinishwa na mamlaka husika”, amesema.

