Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM:KAMPUNI ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC), imesema mwaka mpya wa 2025 itajenga uhusiano bora na vyombo vya habari nchini Tanzania ili kuzitangaza kazi wanazozifanya kuhusu kampuni hiyo kwa viwango vipya.
Kiongozi wa tawi la CCCC nchini, Li Yuliang amesema hayo wakati wa hafla fupi ya wanahabari waliyoifanya ikiwa na lengo ya kutathmini mwaka unaoisha wa 2024, mipango ya 2025 pamoja na kuangalia maeneo yaliyokuwa na upungufu ili yaweze kuboreshwa.
Yuliang amesema, kukutana huko na wanahabari ni jambo zuri na mwanzo mpya wa ushirikiano wa kikazi baina ya pande zote mbili.
Amewashukuru wanahabari wote waliofanya nao kazi kwa mwaka uliopita wa 2024, kwa mchango wa kipekee wa kila chombo kuweza kufanikisha kuripoti taarifa zote za kampuni hiyo, ikiwa ni pamoja na kupokea ushauri wa nini kiboreshwe kwa mwaka unaokuja 2025.
Katika hafla hiyo kila chombo kiliweza kueleza shughuli inazozifanya, imeshiriki vipi katika kuandika habari za kampuni hiyo, na mikakati ya mwaka ujao.
Pia alielezea kuhusu taarifa ya maendeleo ya kampuni hiyo hapa nchini pamoja na miradi yake inayoifanya.
Naye Ofisa Msaidizi Ofisi ya Utawala katika kampuni hiyo ya CCCC, Yu Zixuan amesema pamoja na maendeleo waliyonayo katika soko la Tanzania, vyombo vya habari vimekuwa ni daraja katika maendeleo hayo kupitia usambazaji wa habari zake.
“Vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kuunda taswira ya shirika na kuongeza ufahamu wa umma,” amesema na kuongeza kuwa, hafla hivyo imelenga kujenga jukwaa la mazungumzo baina yake na vyombo vya habari ili kujadili mwelekeo wa maendeleo ya sekta yao.
“Kupitia tukio hili, tunatarajia kufanya kazi pamoja na marafiki zetu wa vyombo vya habari ili kuchangia katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania.
“Kupitia majadiliano ya wazi wazi, tutaimarisha zaidi uhusiano kati ya tawi na vyombo vya habari, kukuza uboreshaji wa jumla wa shirika,” amesema.
Amesisitiza kuwa mwaka huu 2024 ni kumbukumbu ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China na miaka 60 ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania.