Na Danson Kaijage
DODOMA: MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mji wa Bunda (BUWSSA),kwa muda wa miaka minne imepitishiwa miradi ya thamani ya Sh. Bilioni 28.1, mpaka sasa Sh.Bilioni 11.89 tayari zimepokelewa, baadhi ya miradi imekamilika na mingine utekelezaji unaendelea.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa BUWSSA Esther Gilyoma alipokuwa akielezea mafanikio ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma.
Esther amesema miongoni mwa miradi iliyokamilika ni pamoja na wa ujenzi wa chujio la maji Nyabehu – Bunda ambao umegharimu Sh.Bilioni 10.6 , katika mradi huo wananchi 227,446 wananufaika.

Pia amesema Mradi wa Miundombinu ya Majitaka Butakale – Bunda utekelezaji wake umefikia asilimia 46 na unagharimu Sh.Bilioni 1.72 huku wananchi 227,446 wanatarajiwa kunufaika.
Alitaja mradi mwingine ni ujenzi wa Maji Balili, Rubana na Kunzugu – Bunda umekamilika na umegharimu Sh.Milioni 759.8 na wananchi 7,699 wamenufaika.
Mradi wa Ujenzi wa Maji Manyamanyama Mugaja – Bunda, umekamilika ambao umegharimu Sh.Bilioni 1.13 na wananchi 7,012 wamenufaika.

Amesema kuwa Mradi wa ujenzi wa maji Misisi- Zanzibar Mjini Bunda umegharimu Sh.Milioni 733.24 na wananchi 7,042 wamenufaika na huduma ya majisafi na salama huku Mradi wa Kusambaza maji Wariku utekelezaji wake umefikia asilimia 40 na wananchi 33,088 wanatarajiwa kunufaika.
Pamoja na miradi hiyo, amesema kuna Mradi wa kusambaza maji Kisangwa umegharimu Sh.Milioni 716 na wananchi 20,688 wanatarajiwa kunufaika ambapo utekelezaji umeanza na upo asilimia sita.
Mradi wa kusambaza maji Migungani Kaswaka unagharimu Sh.Bilioni 1.2 na watanufaika wananchi 37,058, Mradi wa kusambaza maji Nyamswa Bunda utagharimu Sh.Bilioni 8.3 na watanufaika wananchi 51,935.
Mkurugenzi huyo amesema.Mamlaka ina mipango mbalimbali kwa ajili ya kuhakisha huduma inazidi kuinaimarika mjini Bunda kwa mwaka wa fedha 2025/26 .
.