Na Lucy Ngowi
KATIBU wa Kamati ya Wanawake ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Asha Moto, ameibuka mshindi katika mchujo wa ubunge wa viti maalum mkoa wa Mtwara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika mchujo huo, Asha amewashinda wagombea wengine waliotia nia akiwemo Agnes Hokororo, Dkt. Rahman Hingora, Athumin Mapalilo, Days Ibrahim na Jane Chikomo.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Asha amewashukuru wajumbe wa CCM kwa imani waliyoionyesha kwake na kuwaomba wakazi wa Mtwara kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 28, mwaja huu 2025 kwa ajili ya kuwapigia kura wagombea wa CCM.
“Mimi kama Mbunge wa Viti Maalum nitakayewakilisha mkoa wa Mtwara, nawahakikishia kuwa nitakuwa nanyi bega kwa bega, asubuhi na mchana katika shughuli zote za maendeleo,” amesema.
Amesisitiza kuwa lengo lake ni kushirikiana na wananchi kupambana na umasikini, huku akihimiza nafasi ya mwanamke katika kuimarisha familia na jamii kwa ujumla.
“Tutakuwa nguzo bora kwa familia zetu. Tusimame pamoja kwa maendeleo ya mkoa wetu na taifa kwa ujumla,”amesema.
Wito wake kwa wanawake wa Mtwara ni kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kisiasa ili kuongeza uwakilishi wa wanawake wenye maono na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya.