Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, akisaini kitabu cha wageni katika banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB).
Na Mwandishi Wetu
GEITA: MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amepongeza Bodi ya Bima ya Amana (DIB), kwa kazi inazofanya ambazo ni muhimu katika kuchangia uthabiti wa sekta ya fedha.
Mboni ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la DIB, leo Septemba 22, mwaka huu 2025 katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini ambayo yanaendelea hapa mjini Geita.

Akiwa katika banda hilo, Mboni ameelezwa majukumu ya DIB kwamba ni kusimamia mfuko wa bima ya amana, kulipa fidia kwa wenye amana iwapo benki au taasisi ya fedha itafungwa na kufilisika,
Pamoja na kuendesha shughuli ya ufilisi wa benki au taasisi ya fedha inapoteuliwa kufanya hivyo na Benki Kuu ya Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, akipokea zawadi kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, pembeni yake ni Ofisa Mwandamizi Mkuu wa DIB, Kulwa Kasuka.
Vile vile Mkuu huyo wa Mkoa ameelezwa kwamba kuanzia Julai mwaka huu 2025, DIB itakuwa na jukumu lingine la kupunguza hasara katika benki au taasisi ya fedha ambayo inapitia changamoto katika utendaji wake.