Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuendeleza juhudi za kukuza mafunzo ya amali na stadi za kazi kwa kuhakikisha kunafanyika ufuatiliaji wa karibu katika vyuo vyote vinavyotoa taaluma hiyo, iwe ni vya umma au binafsi.
Vyuo hivyo ni pamoja na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii (FDC), na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Majaliwa ameagiza hayo wakati akifungua kongamano la kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Amesema kuwa elimu ya ufundi stadi ni njia muhimu ya kuwawezesha Watanzania kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia kujipatia kipato, kujiajiri au kuajiriwa, hivyo kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi.
“Tunataka kuongeza ujuzi wa Watanzania. Elimu ya ufundi stadi inapaswa kutolewa kwa kila mtu mwenye nia ya kujifunza, bila kujali kiwango chake cha elimu. Unaweza kuwa na shahada ya chuo kikuu lakini bado ukahitaji ujuzi wa ufundi,” amesema.
Amesisitiza ni lazima wanaohitaji kuwa mafundi katika fani mbalimbali, kama vile umeme, waende kusomea katika vyuo vinavyotoa elimu hiyo kwa vitendo.

“Logic bado iko pale pale kama unataka kuwa fundi umeme, lazima uende kwenye chuo kinachofundisha umeme,” amesema.
Pia amehimiza Wizara ya Elimu kuendelea na juhudi za kuhakikisha vyuo vya FDC na VETA vinaboreshwa na vinatoa elimu bora ya ufundi kwa wote.
Amesisitiza elimu hiyo iwe na mwelekeo wa kuwajengea Watanzania uwezo wa kuchangia kikamilifu maendeleo ya kiuchumi kupitia ujuzi wao.
“Lengo letu ni kuwawezesha Watanzania kupitia elimu ya watu wazima na stadi za kazi ili wajikwamue kiuchumi na kuleta mchango chanya kwa taifa,” amesema Waziri Mkuu.
Ametoa wito kwa taasisi zote zinazotoa mafunzo ya ufundi kushirikiana na serikali katika kuhakikisha elimu hiyo inafikia kila Mtanzania mwenye nia ya kujifunza na kuleta mabadiliko katika jamii.