Kufanya Marekebisho Madogo Ya Katiba Ya Chama
Na Danson Kaijage
DODOMA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza sababu ya kuitisha Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho utakaofanyika kesho kwa njia ya mtandao, ambapo ajenda kuu ni kufanya marekebisho madogo ya Katiba ya Chama.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala, amesema kuwa marekebisho hayo yanazingatia masharti ya Katiba ya CCM, Ibara ya 99(1)(a-f)(2), inayoruhusu kufanyika kwa mkutano huo iwapo kutakuwepo na ulazima wa kikatiba.
“Wanaoweza kufanya marekebisho ya Katiba ya CCM ni Mkutano Mkuu pekee. Na kwa kuwa tumeona kuna umuhimu, ndiyo maana mkutano huu unafanyika kwa ajenda moja tu marekebisho madogo ya Katiba,” amesema Makala.
Ameongeza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakishangaa juu ya mkutano huo kufanyika kwa njia ya mtandao, lakini amesisitiza kuwa huo ni mwenendo wa dunia ya sasa inayokwenda na kasi ya teknolojia.
“Maandalizi yamekamilika. Tuna uhakika kuwa mkutano utafanyika vizuri na kila mtu atashuhudia kupitia mtandao,” amesema.