9Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: RAIS wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mwalimu Suleiman Ikomba ameelezea dhamira yake ya kuwaleta walimu pamoja, kuwatumikia kwa uadilifu, na kuijenga upya taswira ya taaluma ya ualimu kama uti wa mgongo wa taifa.
Ikomba ameelezea hayo alipozungumza na Mfanyakazi Tanzania kuhusu dhamira yake kwa CWT baada ya kuchaguliwa kuwaongoza walimu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030.
Amesema uamuzi wake wa kugombea nafasi ya urais ulitokana na wito wa dhati wa kuwatumikia walimu, licha ya changamoto na mitazamo tofauti iliyokuwepo.
“Miaka mitano ilipofika, tulihitaji viongozi wapya. Nilitafakari sana kabla ya kugombea. Nilijua kabisa kwamba nafasi hizi si za kujitwalia kibinafsi bali ni dhamana ya wanachama.
“Nilikuwa tayari kama nitashinda au kushindwa, kurudi kwenye kazi yangu, lakini dhamira yangu ilikuwa kuhakikisha chama kinakuwa cha wanachama na si cha watu wachache,” amesema.
Ameeleza kwamba kazi kubwa iliyo mbele yake sasa ni kuunganisha walimu wote nchini bila kujali tofauti za kiitikadi, kijiografia au vyeo.
Amesisitiza kuwa maendeleo ya kweli ya walimu hayawezi kufikiwa bila mshikamano wa kweli na mawasiliano ya wazi kati ya uongozi na wanachama.
“Lazima tuwasaidie walimu kwa pamoja. Tuone matatizo yao na tuwaoneshe njia ya kuyatatua. Sisi kama watumishi wa umma, lazima tufikiri njia bora zinazotufaa wote, si kwa masilahi ya wachache,” amesema.
Ikomba amegusia pia kuibuka kwa vyama vingine vya walimu nchini, akisema ni muhimu kuchunguza kiini chake, kusikiliza sababu za kuibuka kwake, na kujifunza.
Amesisitiza kuwa chama cha walimu kinapaswa kusimama kama sauti ya kweli ya walimu wote, na kuhakikisha kila mwalimu anahisi kusikilizwa na kuheshimiwa.
“Lazima tuelewe vyanzo vya migawanyiko. Tujue walimu wana shida zipi hadi wanatafuta sehemu nyingine ya kujiunga. Chama hiki ni cha wanachama tunawajibika kujifunza, kusahihisha, na kuboresha,” amesema.
Pia ametoa ahadi kwa walimu kuwatumikia kwa ukamilifu na kuhakikisha kuwa changamoto zinazowakumba zinapatiwa majibu.
“Nataka kuona walimu wanapata matunda bora ya kazi yao. Nataka kuwaona wakifurahia kazi yao kwa sababu mazingira yao yameratibiwa vizuri. Naomba tushirikiane ili kazi yetu ya ualimu ibaki na hadhi na ubora unaostahili,” amesema.