Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari ameisisitiza Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) kuhakikisha inakamilisha haraka kazi ya ufasili wa sheria zote kwa lugha ya Kiswahili,
Hususan zile zinazohusu uchaguzi mkuu na kanuni zake, kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Amesisitiza hayo katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam

Joharupamesema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza upatikanaji wa haki kwa wananchi kwa kuwawezesha kuelewa sheria zinazoongoza uchaguzi.
“Nafikiri tuendelee kuongeza jitihada katika kazi yetu tunayoifanya ya kufanya ufasili wa sheria, maana kwa kufanya hivyo tutawezesha ufikiwaji wa haki kwa wananchi vizuri hasa hizi sheria za uchaguzi na kanuni zake,” amesema.
Pia ameipongeza Ofisi hiyo kwa kazi nzuri ya utoaji wa elimu kwa umma kupitia maonesho hayo, akisema inasaidia kuwaelimisha wananchi kuhusu utungaji na utekelezaji wa sheria nchini.
Kwa upande wake, Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD, Mariam Possi ameeleza kuwa wananchi wanaotembelea banda hilo wamekuwa wakionesha kiu kubwa ya kuelewa mchakato wa kutungwa kwa sheria, urekebishaji wake, na kazi ya ufasili kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili.
“Katika kipindi chote cha maonesho, tumepokea wadau wengi wa sheria na wananchi kutoka maeneo mbalimbali wanaotaka kujua majukumu ya ofisi yetu na namna ya kuzipata sheria zilizorekebishwa toleo la mwaka 2023 pamoja na zile zinazofanyiwa ufasili kwa sasa,” amesema.
Amesema ufasili wa sheria ni nyenzo muhimu ya kuwezesha jamii kufahamu haki na wajibu wao kwa kutumia lugha inayofahamika na wengi.
Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kutumia njia mbalimbali kuhakikisha sheria hizo zinawafikia wananchi kwa urahisi popote walipo.