Na Danson Kaijage
DODOMA: MAMLAKA ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), imesema inajipanga kuhakikisha gesi asilia inatumika pia kwenye magari.
Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Ushirikiano wa Ndani, Charles Nyangi, amesema hayo kwenye maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma.

Amesema gesi hiyo pia ni muhimu kwa matumizi ya majumbani na viwandani, na hivi sasa inapatikana Mtwara, Lindi na Dar es Salaam.
Amesema Serikali inaendelea kuwekeza ili kusambaza huduma hiyo katika mikoa mingine.
Pia amesema gesi asilia hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa, hasa kwenye sekta ya uzalishaji wa umeme, na kutolea mfano uwekezaji wa Serikali katika miradi ya umeme wa bwawa ambayo inachangia kuongeza upatikanaji wa nishati endelevu.
Amesema kupitia usimamizi wa PURA, Serikali inalenga kuhakikisha kwamba rasilimali za mafuta na gesi asilia zinawanufaisha Watanzania kwa kuimarisha ushirikishwaji wa wazawa, kukuza ujuzi wa kitaifa na kuongeza fursa za kiuchumi.
Amesema PURA imetumia maonesho yanayoendelea jijini Dodoma kuwaelimisha wananchi kuhusu majukumu yake pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta ya mafuta na gesi asilia, hasa mkondo wa juu wa petroli.
“Moja ya majukumu yetu muhimu ni kuhamasisha ushiriki wa wazawa kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli. Ushiriki huu umegawanywa katika maeneo matatu makuu: kupitia ajira, kupitia ujasiriamali kwa maana ya utoaji wa bidhaa na huduma, na kupitia uwekezaji,” ameeleza Nyangi.
Ameongeza kuwa kushiriki kwa PURA katika maonesho hayo kunalenga kuwaelimisha wananchi juu ya majukumu ya mamlaka na namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo muhimu ya kiuchumi.