– Wasema Unarekebisha Nguvu Za Kiume, Kupunguza Uwezekano Wa Kupata Tezi Dume
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MTAALAMU wa Fani ya Maabara katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), kilichopo Mtwara, Oliver Mbemba ameuelezea mwani kama zao bahari linalosaidia kwenye mfumo wa uzazi kwa wanaume na wanawake.
Kwa wanaume amesema zao hilo la mwani linarekebisha nguvu za kiume, ikiwa ni pamoja na kupunguza uwezekano wa kupata tezi dume.
Mbemba amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya miaka 30 ya uanzishwaji wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ( VETA), yanayoendelea Katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Dar es Salaam (JNICC).
Akizungumza kwenye Banda la Maonesho la VETA Mtwara, amesema kwa wanawake inasaidia kurekebisha uiano wa homoni na kuondoa maumivu wakati wa hedhi.
“Pia linasaidia wamama wanaonyonyesha kwenye uzalishaji wa maziwa,” amesema.

Amesema zao bahari hilo lina madini 92 ambayo hufanya kazi mbalimbali katika mwili ikiwemo pia utunzaji wa ngozi, mfumo wa mzunguko wa damu mwilini kwani huweza kurekebisha shinikizo la juu la juu, na shinikizo la chini la damu.
Amesema chuo hicho wamekuwa wakifanya tafiti kwenye udongo na mazao bahari ambayo ni mwani, lakini pia maji salama yanayotumika hospitalini.
” Ni fani kamili mwanafunzi anasoma mwaka wa kwanza mpaka wa tatu, akimaliza atafanya kazi kiwanda chochote,” amesema.
Amesema pia wana bidhaa mbalimbali za mwani ikiwemo unga wake ambao hutumika kwenye chakula, sabuni za kuogea, mafuta ya maji na mgando.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore amesema wataendelea kutoa elimu ya ufundi stadi pamoja na kusimamia bunifu na teknolojia mbalimbali.