Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: SHILINGI Bilioni 27 zimetolewa na Serikali ya Japan nchini Tanzania kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya nchini.

Akisaini mkataba wa msaada huo jijini Dar es salaam leo Machi 14, 2025 Katibu mkuu wizara ya Fedha, Dkt Natu Mwamba amesema fedha hizo zitatumika katika ununuzi wa vifaa-tiba ili kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto hapa nchini.
Amesema ufadhili huo unaendana na Mpango wa sasa wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaolenga kutatua changamoto za ubora katika utoaji huduma za afya nchini.

“Ufadhili huu unaunga juhudi za Serikali ya Tanzania kwenye sekta ya afya, zinazolenga kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wakati kwenye jamii,” amesema.
Dkt Mwamba amesaini nyaraka mbili ambazo ni kati ya Wizara ya Fedha na Ubalozi wa Japan na nyingine kati ya Wizara ya Fedha na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).
Kwa upande wa Tanzania mradi huo utatekelezwa na Wizara ya Afya.
“Utekelezaji wa mradi huu utaboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma bora za afya hususani Huduma ya Mama na Mtoto kwa kutoa vifaa-tiba vya kisasa vitakavyoongeza uwezo wa kufanya uchunguzi na matibabu,” amesema.
Ametaja hospitali saba za Rufaa ambazo mradi utatekelezwa kuwa ni hospitali ya Dodoma, Hospitali ya Tumbi iliyoko mkoa wa Pwani, Hospitali ya Mount Meru iliyoko Arusha, Hospitali ya Sekou-Toure iliyoko Mwanza.
Nyingine ni Hospitali ya Songea iliyoko Ruvuma, Hospitali ya Maweni iliyoko mkoani Kigoma na Hospitali ya Lumumba iliyoko Zanzibar.
Amesema msaada huo ni mwendelezo wa ushirikiano unaokuwa kati ya nchi zetu mbili kama inavyodhihirishwa na kuongezeka kwa namba ya miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia misaada na mikopo nafuu.
Naye Balozi wa Japan nchini, Yoichi Mikami amesema msaada huu utasaidia kuanzia ngazi za chini, kwamba Japan imekuwa ikitoa misaada katika sekta ya afya ili kuchochea maendeleo.
“Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuweza kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi na kuboresha Maisha ya Watanzania,” amesema.
Kwa upande wa Mwakikishi Mkuu wa JICA nchini Tanzania, Hitoshi ARA amesema JICA imekuwa mstari wa mbele kusaidia sekta ya afya nchini, Hitaji la Vifaa vya Matibabu katika Hospital za Kanda.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ismail Rumatila amesema hospitali hizo zitaweza kutoa vifaa-tiba vya kisasa vitakavyoongeza uwezo wa kufanya uchunguzi na matibabu.
“Tunaishukuru serikali ya japan kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania hasa katika sekta ya afya,” amesema.