Na Lucy Ngowi
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limetoa tahadhari kwa wadau wote wa usafiri kwa njia ya maji, na wanaofanya shughuli za kiuchumi baharini na kwenye maziwa, kuchukua tahadhari kutokana na kuwepo kwa upepo mkali kwa siku tatu mfululizo kuanzia jana hadi kesho.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu TASAC, imetoa tahadhari hiyo baada ya kupokea taarifa ya upepo huo kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ( TMA).
Kwa mujibu wa taarifa ya TASAC, TMA imeeleza kuwa kuna uwezekano upepo huo mkali unaozidi kilomita 40 kwa siku tatu mfululizo kuanzia Septemba mosi hadi tatu mwaka huu.
Maeneo yatakayoathiriwa ni yale ya Ukanda wa Pwani ya Kusini mwa Bahari ya Hindi katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, baadhi ya maeneo ya Kusini mwa Ziwa Tanganyika katika mikoa ya Rukwa na Katavi.
Pia maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini mwa Bahari ya Hindi katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani ikijumuishwa Visiwa vya Mafia pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba.
Taarifa imetaja athari zinazoweza kujitokeza kuwa ni kuathitlrika na kughairishwa kwa baadhi ya shughuli za baharini na kuharibika kwa miundombinu ya bahari.
TASAC inawataka wadau wake hao kuchukua tahadhari hiyo mpaka TMA itakapotangaza hali ya hewa kuwa shwari ili kuzuia ajali zitakazohatarisha maisha ya wavuvi na wasafiri.