Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Reli Tanzania(TRC) limesema treni ya abiria namba Y14 ikiwa na kichwa Cha treni namba 9002,mabehewa 12 ya abiria,behewa Moja la vifurushi na behewa moja la breki limepata ajali kati ya stesheni ya Kazuramimba na Uvinza mkoani Kigoma na kusababisha majeruhi 70.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Jamila Mbarouk ajali hiyo imetokea majira ya Saa 7:30 usiku usiku wa kuamkia leo Agosti 28,2024.
Amesema ajali imetokea baada ya mabehewa sita ya treni kuacha njia ambapo kati ya majeruhi 70 wanawake ni 26 na wanaume ni 44.
Amesema treni ilikuwa na jumla ya abiria 571 wakisafiri kutoka Kigoma kuelekea mikoa ya Tabora,Dodoma,Morogoro,Pwani na Dar es Salaam.
Amesema TRC kwa kushirikiana na kitengo Cha Afya Cha mkoa wa Kigoma walipeleka majeruhi katika Hospitali ya wilaya ya Uvinza Kwa ajili ya matibabu.
“Hali za afya za abiria zinaendelea kuimarika,majeruhi 57 tayari wamwruhusiwa,name wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Uvinza na watano wamehamishiwa Hospitali ya Maweni,” amesema.
Aidha amesema treni iliendelea na safari kuelekea mkoa wa Tabora,Dodoma,Morogoro,Pwani na Dar es Salaam.
Amesema shirika linawapa pole majeruhi na linaendelea na jitihada za kuwahudumia majeruhi na hakuna taarifa ya vifo vilivyotokana na ajali hiyo.