Na Lucy Ngowi
TUME ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), imeagizwa kutoa mafunzo ya Mfumo wa Uendeshaji na Usimamizi wa Mashauri kwa Njia ya Mtandao kwa wafanyakazi, waajiri, mawakili, wawakilishi binafsi na jamii yote waelewe umuhimu na matumizi yake.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Protrobas Katambi ameagiza hayo wakati wa ufunguzi wa nafunzo ya mfumo huo kwa wadau wa tume hiyo.

Katambi amesema, mfumo huo ni mkakati wa serikali sio wa kurahisisha huduma kwa wananchi pekee, bali kusogeza huduma za utatuzi wa migogoro karibu na wananchi.
“Mara kadhaa serikali kupitia wizara yetu imepambania sana bungeni kuhakikisha mradi huu unakamilika.
“Na Kamati ya Bunge, Ustawi na Maendeleo ya Jamii inasubiri kwa hamu kuona mfumo huu unaanza kazi maana imekuwa ikituhoji na kutufuatilia kwa karibu,” amesema.
Maelezo yake ni kwamba, baada ya mafunzo ya wadau, tume hiyo itapanga siku ya kuipitisha kamati hiyo kwenye mfumo kabla ya kuanza matumizi ili wabunge wapate uelewa wa namna mfumo utakavyofanya kazi na kuleta tija kwa wananchi hususani wadau wa haki-kazi.

Awali Mkurugenzi wa CMA, Usekelege Mpulla amesema, mafunzo hayo ni utekelezaji wa maagizo na mkakati wa serikali na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan akisisitiza kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Pia Rais Samia amesisitiza kutumia mifumo inayosomana, vike vile upatikanaji wa huduma ama migogoro ya kazi kwa haraka.