Na Mwandishi Wetu Arusha
KATIBU Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Musa amewataka Maofisa Tarafa na Watendaji wa Kata kuwa wabunifu katika kusimamia uwajibikaji na kuongeza vyanzo vya miradi kutokana na fursa zilizopo kwenye maeneo yao.
Missaile ametoa kauli hiyo leo Agosti 08 , 2024 Jijini Arusha wakati akifungua mafunzo kwa Maofisa Tarafa na Watendaji wa Kata katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Amewataka Viongozi na Watendaji hao kuwa wabunifu wa vyanzo vya mapato ya Serikali na kuhimiza uwajibikaji wa watumishi.
“lakini mara nyingi tumekuwa hatuna ubunifu wa usimamizi na uwajibikiaji, tuna fursa nyingi za kiuchumi lakini hatuna ubunifu, hatusimamii, fursa za kijamii zinazopatikana kule hatuzielezei vizuri” alisema Missaile Musa.
Amesema uwepo kwa changamoto zinazotokana na kutozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika utendaji kazi wa kila siku kwa viongozi na watendaji hao katika ngazi ya msingi zitapata suluhu baada ya mafunzo hayo hususani masuala ya maadili, uzalendo na masuala ya kiutumishi.
Aidha, amewataka kuelewa majukumu yao kwa kina ili kuepuka muingiliano wa kimajukumu lakini pia kwa Maafisa Tarafa kufahamu masuala ya kisera na kuhimiza utekelezaji wake na Watendaji Kata kuandaa Mpango kazi wa Kata ili kuwa na agenda ya pamoja katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Naye Ibrahim Minja Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema mafunzo hayo ya siku mbili yanatolewa na ofisi yake kupitia Programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Regions and Local Government Strengthening Programme-RLGSP), kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na Chuo cha Utumishi wa Umma.
Amesema jumla ya washiriki 181 ambao ni Watendaji wa Kata 157 na Maafisa Tarafa 23 wanatarajiwa kupatiwa mafunzo hayo ili kwenda kuimarisha utendaji wao wa kazi kwenye maeneo yao.
Aidha, amesema katika awamu hii ya mwisho inahusisha mikoa nane ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya na Ruvuma ambapo Maafisa Tarafa 203 na Watendaji wa Kata 1,377 watapatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo.
Kwa upande wake Edward Nguni Mtendaji wa Kata ya Naikanuka Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro amesema mafunzo hayo yatamwongezea weledi wa kazi na kuboresha ushirikiano na watumishi wa Sekta zote katika eneo lake yeye akiwa kiungo muhimu Pamoja na kuweza kutatua kero na migogoro ya wananchi kabla ya viongozi kufanya ziara katika eneo lake.