Na Lucy Ngowi
“HAYA maonesho tumeyapa umuhimu wake kwa sababu tulidhamiria kushinda. Sio mara ya kwanza kupata ushindi. Tumeweka bidii na tulidhamiria tutashinda,”.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajab Mabele amesema hayo muda mfupi baada ya kutangazwa washindi wa kwanza wa jumla katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yajulikanayo kama 88, yaliyofanyika mkoani Dodoma.
Amesema katika maeneo ya kilimo, ufugaji na uvuvi wamekuwa wakiyafanya kitaalamu, na ni maeneo wanayoshughukika nayo siku zote kwa mwaka.
Amesema JKT limepata ushindi wa kwanza wa jumla katika maonesho hayo kutokana na bidii waliyoionesha katika maandalizi ya maonesho hayo.
“Mahali hapa sisi ni pa kudumu, na siyo tupo wakati wa maonesho tu, na ushindi wowote ni bidii,hata mwanafunzi anapokuwa shuleni ,ili afanye vizuri anatakiwa kufanya bidii na ndiyo maana tumechukua ushindi huu na hata mwaka jana hapa Dodoma tulishinda nafasi ya kwanza,”amesema.
Amesema, “Katika kilimo,tunaonesha kilimo bora,katika mazao ya bustani tunalima kitaalam ,lakini pia katika eneo la mifugo nako tunao ng’ombe wetu na mifugo mingine ambayo pia tunafuga kitaalam,
“Ukija katika eneo la uvuvi na ufugaji hali kadhalika tunafanya vizuri,tunazo teknolojia ya ufugaji samaki wa matenki ambao sisi JKT ndiyo tulianzisha Teknolojia hii na kuipeleka katika maonesho mbalimbali ambayo sasa hivi inafanywa na wengi.”amesema Meja Jenerali Mabele.