Na Lucy Ngowi
SHERIA ya Ajira na Mahusiano Kazini imekuwa ikichanganya watumishi,hali inayosababisha ucheleweshaji wa kumaliza migogoro ya wafanyakazi.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), Edo Makata amesema hayo alipozungumza na Gazeti la Mfanyakazi.
Amesema kutoka na mkanganyiko huo, wafanyakazi wenye migogoro na mwajiri wanaweza kukaa miaka mitatu mpaka minne hawajapata majibu yao.
“Ama unakuta mfanyakazi anaweza kurudishwa kazini lakini mwajiri wake anakuwa hamhitaji,” amesema.
Amesema changamoto hiyo imejitokeza kwa wafanyakazi waliondolewa ambao hawakuwa na vyeti vya elimu ya kidato cha nne.
Kwamba waliokuwa Wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), wamekumbwa na changamoto kutokana na shirika hilo huko nyuma kuajiri wasiokuwa na sifa ya cheti cha kidato cha nne.
“Ilipofika muda wa kutekeleza matakwa ya serikali kwa nyaraka mbalimbali zilizotumwa TRC,wafanyakazi wengi waliondolewa wasiokuwa na elimu ya kidato cha nne, pia wasiokuwa na vyeti.
“Hii ilikuwa ni shida sababu wameshaajiriwa, wamekaa humo, ila matakwa ya serikali kwa mujibu wa nyaraka, walihitajika watoe vyeti vyao. Hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa sababu walioondolewa kwenye mshahara hawakujua hatma yao.
“Hizi kesi zimekuwa ni nyingi zimeendelea kupelekwa kwenye Tume ya Utumishi wa Umma kama chombo ambacho kinasikiliza rufaa ambazo zinaendelea kwa watumishi wa umma kwa sababu sekta zote mbili zimeonekana sekta za umma kwa asilimia 100,” amesema.
Pia ameeleza changamoto nyingine kwa watumishi wanaofukuzwa kazi kwa sababu mbalimbali, endapo kesi itapelekwa Tume ya Utumishi wa Umma, na ikatokea mfanyakazi ameshinda, mwajiri hukata rufaa kwa Rais.
Amesema mwajiri anapokata rufaa huchukua muda mrefu kuiamua huku mfanyakazi anasota bila ajira japo tume imeamua arejeshwe kazini.
Akizungumzia upande wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), wafanyakazi wengi walipeleka kesi zao Tume ya Usuluhishi na Upatanishi, lakini kupitia mahakama kesi hizo zilionekana zimepelekwa Tume ya Utumishi wa Umma.
“Sasa tume inakaa muda mrefu kuweza kufanya maamuzi yake kwa muundo wake,” amesema.