Na Mwandishi Wetu
Wapiga kura waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wataweza kutumia simu zao ndogo za mkononi jina maarufu vitochi ama viswaswadu kuanzisha mchakato wa kuboresha au kuhamisha taarifa zao.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani amesema hayo leo Julai 18 kupitia taarifa yake aliyoitoa.
Taarifa hiyo inasema uamuzi huo wa Tume umetokana na maoni ya wadau wa uchaguzi.
“Tume imefanyia kazi maoni na ushauri huo na kuanzia Julai 20 Julai, 2024 watu wote wenye simu za kawaida maarufu kama kitochi au kiswaswadu na watahitaji kuboresha au kuhamisha taarifa zao, watapata huduma hiyo kwa kupiga USSD Code *152*00# na kubonyeza namba tisa.
Baada ya hapo wataendelea na hatua nyingine kama itakavyokuwa inaelekezwa kwenye simu husika,” imesema.
Maelezo ya taarifa hiyo ni kwamba mpiga kura anayetumia njia hiyo atapokea namba maalum kupitia simu yake kisha atalazimika kwenda na namba hizo kwenye kituo anachotarajia kutumia kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ili kukamilisha mchakato na kupewa kadi mpya.
Katika hatua nyingine, Tume imetoa taarifa kwa umma kuhusu kuanza rasmi kwa kituo cha huduma kwa mpiga kura kinachoanza kutoa huduma kuanzia leo Julai 8, Julai, 2024.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Kailima, huduma hiyo ni ya bure na itatolewa kwa saa 14 kila siku kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 2:00 usiku.