Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Ujenzi Sports Club imeendelea kuunga mkono juhudi za kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa wanafunzi wa shule ya msingi Mlezi jijini Dodoma.
Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya juhudi za Ujenzi Sports Club kuunga mkono kazi inayofanywa na shule hiyo katika kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wanafunzi wengine kupata mazingira bora ya kujifunzia.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na madaftari, vyombo vya kulia chakula, vifaa vya usafi, sabuni, ndoo pamoja na fedha kwa ajili ya ununuzi wa mipira ya michezo.
Akikabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Ujenzi Sports Club, Ibrahim Chatila, amesema klabu hiyo inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na walimu katika kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kutimiza ndoto zao kielimu na katika maisha kwa ujumla.

Amesema msaada huo ni sehemu ya jitihada za Ujenzi Sports Club kuunga mkono juhudi zinazofanywa na shule hiyo, huku akiahidi kuwa klabu itaendelea kushirikiana na kuwahamasisha wadau wengine, hususan katika sekta ya ujenzi, kujitokeza na kusaidia juhudi hizo.
“Tunatambua kazi kubwa inayofanywa na walimu katika kuwalea na kuwawezesha watoto hawa. Msaada huu ni sehemu ya mchango wetu katika kuunga mkono juhudi hizo, na tutaendelea kuwahamasisha wadau wengine kujitokeza na kusaidia,” amesema Chatila.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mlezi, Magreth Kisanga, ameishukuru Ujenzi Sports Club kwa ukarimu na moyo wa kujitolea uliouonyesha kwa kuwasaidia wanafunzi hao.
Amesema msaada huo utasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa baadhi ya vitendea kazi vinavyohitajika katika kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia na kuishi shuleni.
Kwa upande wake, mwalimu anayesimamia kitengo cha wanafunzi wenye mahitaji maalum, Hashim Msemo, amesema wanafunzi hao wamekuwa wakifanya vizuri katika masomo yao na wameendelea kufanya vyema katika mitihani yao.

Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza na kuunga mkono juhudi za shule hiyo ili kuongeza fursa na mazingira bora kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Shule ya Msingi Mlezi ni shule jumuishi inayotoa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wanafunzi wengine, kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata fursa sawa ya elimu na maendeleo.



