Na Lucy Lyatuu
JESHI la Zima Moto na Uokoaji limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya nishati safi ya kupikia, hususan gesi ya kupikia, pamoja na njia sahihi za kuzuia na kukabiliana na majanga ya moto.
Elimu hiyo imetolewa katika Maonesho ya Nane Nane jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu usalama wa moto katika maeneo ya makazi, biashara na shughuli mbalimbali za uzalishaji.

Jeshi hilo limeeleza kuwa limeona umuhimu wa kutoa elimu hiyo katika Maonesho ya Nane Nane kutokana na maonesho hayo kukutanisha maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara, wafugaji, wajasiriamali na wadau wa sekta mbalimbali.
Kwa kutumia jukwaa hilo, wananchi wamepata fursa ya kujifunza kwa vitendo namna ya kutumia majiko ya gesi kwa usalama, kutambua vihatarishi vinavyoweza kusababisha moto na kuchukua hatua za tahadhari kabla ya janga kutokea.

Katika utoaji wa elimu hiyo, wananchi wamefundishwa namna sahihi ya kutumia na kuhifadhi mitungi ya gesi, kuhakikisha vifaa vya gesi vinafungwa na kutumika kwa usahihi, pamoja na kuchukua tahadhari wanapobaini dalili za kuvuja kwa gesi.
Aidha, wamepewa elimu kuhusu hatua za awali za kuchukua pale moto unapotokea na umuhimu wa kuwa na vifaa vya kuzimia moto katika maeneo yanayohitaji ulinzi huo, huku wakisisitizwa kutotumia njia zisizo salama ambazo zinaweza kuongeza madhara.
Jeshi la Zima Moto na Uokoaji limeendelea kusisitiza kuwa kinga ni hatua muhimu zaidi katika kupunguza madhara yatokanayo na majanga ya moto, hivyo wananchi wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu vyanzo vya moto na namna ya kuvizuia.




