Na Lucy Lyatuu,Dodoma
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeelekeza Mamlaka Ya Mapato Tanzania (TRA) kuchukua hatua za haraka kurekebisha mapungufu yote yaliyoibuliwa na Mdhibiti Na Mkaguzi Mkuu Wa Hesabu Za Serikali CAG, hususan katika maeneo ya ukusanyaji wa kodi na usimamizi wa mapato ya serikali.
Mwenyekiti wa PAC, Devotha Minja, amesema hayo baada ya Kamati kukutana na Menejimenti ya TRA kwa ajili ya kupokea, kupitia na kuchambua taarifa ya hesabu za taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2025, zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Katika kikao hicho, PAC imeielekeza TRA kuchukua hatua za haraka kurekebisha mapungufu yote yaliyoibuliwa na CAG, hususan katika maeneo ya ukusanyaji wa kodi na usimamizi wa mapato ya serikali.
Akizungumza, Minja ameeleza kuwa Kamati imeitaka TRA kuimarisha mifumo yake ya usimamizi wa kodi kwa kuongeza ufanisi katika ukaguzi, uhakiki wa taarifa za walipakodi, pamoja na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa mapato ili kuhakikisha hakuna upotevu wa fedha za umma.
Amesema Kamati inamtaka Ofisa Maduhuri kuwasilisha taarifa ya kiasi cha kodi kilichokusanywa kufikia June 30,2024 na June 30,2025 na taarifa hiyo ifanyiwe usahihi na CAG na kuwasilishwa Kwa Kamati ifikapo Agosti 30,2026.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema taasisi hiyo imepokea maelekezo yote ya PAC na kuyapa kipaumbele, na akiahidi kuwa mapungufu yaliyobainishwa yatashughulikiwa ndani ya muda uliopangwa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Uledi Mussa, amesema kikao hicho kimekuwa fursa muhimu ya kujifunza na kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na walipakodi.
Ameongeza kuwa lengo la TRA ni kuwa taasisi inayoaminika na wananchi, huku ikiendelea kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari kama njia ya kuongeza mapato ya ndani na kuchochea maendeleo ya taifa.
Kadhalika ameiomba PAC kuendelea kuwa mabalozi wa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari .


