Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHAMA cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimewataka wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuhakikisha wanahabari wote wanasajiliwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na mfuko huo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wanachama wa JOWUTA kuhusu haki za fidia kwa wafanyakazi yaliyofanyika Mei 25, 2025 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma, amesema waajiri wana wajibu wa kuzingatia sheria za kazi kwa kuwapatia wanahabari ajira za kudumu au mikataba rasmi.

Amesema kukosekana kwa usajili na mikataba ya ajira kunawanyima wanahabari haki muhimu, ikiwamo huduma za matibabu, fidia ya ulemavu, msaada wa mazishi na mafao kwa wategemezi pale mfanyakazi anapofariki akiwa kazini.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya JOWUTA na WCF, yamewakutanisha wanachama kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu haki za wafanyakazi katika sekta ya habai

Amesema mafunzo hayo ni mwanzo wa mpango wa kutoa elimu hiyo katika kanda nyingine za nchi, ikiwamo Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.
Aidha, ameipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kazi kwa jitihada za kushughulikia changamoto za wanahabari nchini.
Amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wanahabari hawana ajira za kudumu, hali inayohitaji hatua za haraka za kisheria na kiutendaji ili kulinda haki zao.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya JOWUTA na WCF, yamewakutanisha wanachama kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu haki za wafanyakazi katika sekta ya habai



