Na Lucy Lyatuu, Dodoma
TIMU ya Bunge SC imekabidhiwa vifaa mbalimbali vya michezo na Kampuni ya Smart Sport ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mashindano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu 2026.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa timu hiyo, Rebecca Msemwa aliishukuru kampuni hiyo kwa msaada walioutoa, akisema utasaidia kuongeza morali kwa wanamichezo na kuboresha maandalizi ya timu.

Amesema timu hiyo hushiriki mashindano mbalimbali ya michezo na maandalizi ya mashindano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanaendelea vizuri huku wakitarajia kufanya vizuri na kurejea na vikombe.
“Mashindano haya hutuweka pamoja na kutupa nafasi ya kushauriana mambo mbalimbali ya maendeleo ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki. Tunaomba wadhamini zaidi wajitokeze kwa kuwa mahitaji ya vifaa vya michezo bado ni makubwa,” amesma Msemwa.

Aidha, amewataka wachezaji kujitokeza kwa wingi mazoezini ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika mashindano hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Smart Sport, George Wakuganda amesema kampuni hiyo imeamua kutoa msaada huo ili kusaidia maandalizi ya timu hiyo kwa kuamini kuwa vifaa bora vina mchango mkubwa katika ushindi.
“Lengo letu ni kuhakikisha wanamichezo wanakuwa na vifaa bora vitakavyowasaidia kufanya vizuri zaidi,” amesema Wakuganda.
Amesma Smart Sport imekuwa ikiunga mkono michezo mbalimbali nchini ikiwemo SHIMIWI, SHIMUTA pamoja na mashindano ya Mei Mosi, ambapo kampuni hiyo ilipata tuzo kutoka kwa Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho hayo.

Wakuganda amesema vifaa vilivyotolewa vinajumuisha jezi, mipira na vifaa vya michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, basketball, volleyball pamoja na mchezo wa kuvuta kamba.
“Kimsingi mahitaji ya msingi tumeyakidhi, sasa jukumu limebaki kwa timu kufanya vizuri katika mashindano,” amesema Wakuganda.

