Na Mwandishi Wetu, Longido
WANAFUNZI wa shule za msingi katika Wilaya ya Longido mkoani Arusha, wakiwemo wanafunzi wa Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Waliokosa (MEMKWA), wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa chakula shuleni hali inayotajwa kuathiri maendeleo yao ya kitaaluma.
Changamoto hiyo imebainishwa katika kikao cha Jukwaa la Wadau wa Elimu wilayani humo kilichoandaliwa na Shirika la Utafiti, Maendeleo na Huduma za Jamii (CORDS), kikihusisha viongozi wa halmashauri, waratibu elimu, viongozi wa vijiji, walimu pamoja na asasi za kiraia.
Akizungumza katika kikao hicho, Ofisa Elimu wa Kata ya Ngarenaibo, Paulo Teveli amesema baadhi ya wazazi hawapeleki chakula shuleni jambo linalochangia wanafunzi kushindwa kufanya vizuri darasani.
Amesema tatizo hilo linachangiwa na baadhi ya wazazi kutothamini elimu huku wengine wakikabiliwa na hali ngumu ya maisha.

“Tatizo hili linaathiri hata wanafunzi wa MEMKWA ambao katika kata yangu wako 31.
“Tunahitaji ushirikiano wa wadau wote kulitatua, huku tukithamini msaada tunaoupata kutoka CORDS katika sekta ya elimu,” amesema Teveli.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Longido, Sein Kitomali amesema wanafunzi wengi hutembea umbali mrefu kufika shule hivyo wanahitaji chakula na vifaa muhimu vya kujifunzia ili waweze kuzingatia masomo yao.
Amesema shule hiyo ina wanafunzi 62 wa MEMKWA, ambapo 38 wanatarajiwa kufanya mtihani wa darasa la nne mwaka huu.

Amebainisha kuwa msaada wa CORDS umechangia kuboresha mazingira ya kujifunzia kupitia utoaji wa vifaa mbalimbali vya shule.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngoswaki, Karia Mollel amesema jamii za wafugaji bado zina changamoto ya kuthamini elimu, lakini juhudi zinaendelea kuhamasisha wazazi kuwapeleka watoto shule na kuzuia ndoa za utotoni.
Meneja Elimu wa CORDS, Ezekiel Piniel amesema shirika hilo linaendesha Mradi wa Kupambana na Umasikini kupitia Elimu na Uwezeshaji wa Kiuchumi (BELIEF), unaofadhiliwa na Shirika la Stromme Foundation.
Amesema kupitia mradi huo, shule za Ngoswaki na Longido zinapatiwa vifaa vya kujifunzia, kuboreshwa miundombinu pamoja na kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Aidha, vijana na vikundi vya wajasiriamali vinawezeshwa kupitia mafunzo ya stadi za maisha na usimamizi wa miradi.
Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Longido, Nestory Dagharo amesema wazazi wanapaswa kuchangia chakula shuleni kwa kuwa ni sehemu ya wajibu wao katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.

