Na Lucy Ngowi
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji amesema huduma ya kudungwa na nyuki kwa ajili ya kuongeza kinga ya mwili ni moja ya vivutio vinavyopatikana katika maonesho yaliyoandaliwa na wizara hiyo kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Dkt. Kijaji amesema hayo baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho pamoja na wabunge wengine mara baada ya kuwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni.
Amesema maonesho hayo yanalenga kuwaonesha wabunge na wananchi vivutio vya utalii pamoja na huduma mbalimbali zinazopatikana nchini, zikiwemo zinazotokana na mazao ya nyuki.

“Tunawaonyesha watu kwa vitendo vivutio mbalimbali tulivyobarikiwa navyo ndani ya taifa letu. Hata huduma ya kudungwa na nyuki kwa ajili ya kuongeza kinga ya mwili inapatikana hapa,” amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, amesema ongezeko la watalii kwa asilimia 10.2 ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia kampeni mbalimbali za utalii.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, maonesho hayo pia yanalenga kuwafanya wabunge kuwa mabalozi wa utalii katika majimbo yao kwa kuwahamasisha wananchi kutembelea vivutio vya ndani ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani.

“Tunataka wabunge wakawe mabalozi wazuri wa kueleza wananchi kuhusu vivutio tulivyonavyo na umuhimu wa kuendeleza utalii wa ndani,” amesema.
Dkt. Kijaji amesema wizara hiyo imewasilisha utekelezaji wa ahadi ilizotoa mwaka 2025 kwa kuonyesha kwa vitendo mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo.
Ameongeza kuwa katika banda la Bodi ya Utalii Tanzania ( TTB), kuna teknolojia maalumu inayomwezesha mtu kuona wanyama waliopo porini na maeneo mbalimbali ya utalii ikiwemo Ngorongoro Conservation Area, jambo lililowavutia wengi waliofika kwenye maonesho hayo.


