ZANZIBAR: RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametembelea banda la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika Tamasha la Kizimkazi, ambapo alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba.
Rais, pamoja na kutembelea banda la NSSF, ametembelea mabanda ya taasisi mbalimbali na kujionea huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Rais alifurahishwa na kazi inayofanywa na NSSF, hususan katika kuboresha huduma kwa wanachama wake.
Katika hatua nyingine, NSSF imeendelea kutekeleza wajibu wake kwa jamii katika maeneo ya elimu, afya, michezo, mahitaji maalum na kushirikiana na wadau wa maendeleo.

Katika Tamasha la Kizimkazi, Mfuko umetoa majiko janja aina ya 80L Electric Pressure Cooker kwa shule za sekondari.
Majiko hayo yanatumia umeme kidogo, wastani wa ‘units’ mbili kwa saa nzima, ni salama na hujizima baada ya chakula kuiva.
Aidha, NSSF imeshiriki pamoja na wadau wengine wa maendeleo katika Kongamano la Nishati Safi lililofanyika Kizimkazi.
Utoaji wa majiko hayo na ushiriki wa NSSF katika Kongamano la Nishati Safi unaonesha dhamira ya Mfuko kuunga mkono Ajenda ya Kitaifa ya Nishati Safi ya Kupikia, inayolenga kuongeza matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kuboresha afya, kulinda mazingira na kuchochea maendeleo endelevu.

