Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Jimbo la Ngorongoro, Yanick Ndoinyo, ameiomba Serikali kuongeza uwekezaji katika Wilaya ya Ngorongoro, hususan eneo la Loliondo, kwa kufungua miundombinu ya usafiri itakayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.
.
Ametoa ombi hilo alipokuwa akichangia hotuba ya Wizara ya Uchukuzi bungeni, ambapo amepongeza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta za bandari, reli, usafiri wa anga pamoja na miundombinu mingine ya usafirishaji.
Ndoinyo amesema Loliondo ni eneo lenye fursa kubwa za kiuchumi lakini bado halijatumika ipasavyo kutokana na ukosefu wa miradi ya kimkakati.
Ameeleza kuwa bila uwekezaji mkubwa katika sekta ya usafiri, wananchi wa eneo hilo hawataweza kunufaika kikamilifu na kasi ya maendeleo inayotekelezwa nchini chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mbunge huyo ameisisitiza Wizara ya Uchukuzi kuujumuisha Uwanja wa Ndege wa Waso katika mipango ya maendeleo ya wizara hiyo, akisema uwanja huo una umuhimu mkubwa kwa Wilaya ya Ngorongoro ambayo hadi sasa bado haina barabara za lami.
Amesema kukamilika kwa uwanja huo kutasaidia kuongeza ajira kwa vijana, kukuza biashara na kuimarisha sekta ya utalii kwa kuwa eneo la Waso ni kitovu muhimu kinachounganisha vivutio vya utalii vya Serengeti, Ngorongoro na Ol Doinyo Lengai.
Ndoinyo amesema uwepo wa uwanja huo utafungua uchumi wa Ngorongoro na kuifanya wilaya hiyo kuwa kitovu muhimu cha utalii na biashara,
Huku akisisitiza kuwa anaunga mkono hoja ya Wizara ya Uchukuzi kwa kuwa inalenga kuleta mageuzi makubwa katika uchumi wa Tanzania.

