Na Lucy Ngowi
MWENYEKITI wa Bunge Bonanza Festo Sanga amesema kuwa maandalizi ya mbio za Bunge Marathon zinazotarajiwa kufanyika Aprili 18 mwaka huu katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 100, huku akisema kilichosalia kwa sasa ni ujio wa washiriki.
Akizungumza jana na waandishi wa habari Bungeni jijini Dodoma, mwenyekiti huyo alisema kuwa huu ni msimu wa tatu wa Bunge Marathon, tukio ambalo limeendelea kukua na kuvutia washiriki wengi zaidi kila mwaka.
Amesema kuwa wadhamini wakuu wa mashindano hayo ambao ni Silent Ocean, wamehakikisha maandalizi yote muhimu yanakamilika kwa wakati, ikiwa ni pamoja na vifaa vya mashindano na vituo vya usajili pamoja na ugawaji wa vifaa kwa washiriki.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, vituo vya usajili vimeandaliwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mlimani City jijini Dar es Salaam, Ofisi za Bunge , Capital Park, Jamhuri, Shoppers pamoja na Safina House jijini Dodoma, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa washiriki.
Amebainisha kuwa hadi kufikia asubuhi ya leo (jana), zaidi ya washiriki 4,600 walikuwa tayari wamejisajili kushiriki mbio hizo , huku usajili ukiendelea kwa gharama ya shilingi 40,000.
Aidha alisema, makundi yanayojisajili kwa pamoja yanapata punguzo la asilimia 10.
Mbio hizo zitahusisha umbali wa kilomita 5, 10, 15 na 21, ambapo washiriki wote watapatiwa medali, huku washindi wakitarajiwa kujinyakulia medali maalum na zawadi mbalimbali za fedha taslimu.
Katika kipengele cha kilomita 5, mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 2, wa pili shilingi 1,000,000 na wa tatu shilingi 500,000, huku washiriki watakaoshika nafasi ya nne hadi ya kumi nao wakipata zawadi.
Kwa upande wa kilomita 10 na 21, mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 6, wa pili milioni 3 na wa tatu milioni 1.5.
Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo akisisitiza kuwa ni riadha ya Watanzania wote, inayolenga kuimarisha uhusiano kati ya Bunge na wananchi.
“Njoo ukimbie na mbunge wako,kila mwananchi ana fursa ya kushiriki,hii ni riadha ya Watanzania wote,” alisisitiza.
Ameeleza kuwa jitihada hizi zinaungwa mkono na Mheshimiwa Spika wa Bunge kwa lengo la kulifanya Bunge kuwa karibu zaidi na wananchi waliowachagua.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, Rogath Akhwar, ameipongeza Bunge Marathon akisema kuwa mwaka huu tukio hilo limepandishwa hadhi na kufikia kiwango cha kimataifa.
Amesema tayari mwaliko umetumwa kwa nchi wanachama na baadhi yao wameanza kujisajili kushiriki mashindano hayo, hatua inayotarajiwa kuongeza ushindani na ubora wa mbio hizo.
Aidha amewasihi wabunge wametakiwa kuhamasisha wanafunzi wanaoshiriki mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA kushiriki Bunge Marathon ili waweze kuonyesha vipaji vyao na kukuza sekta ya riadha nchini.
Alisema,Mashindano hayo yanatarajiwa kuwashirikisha pia mabingwa mbalimbali wa mbio za marathon pamoja na washindi wa medali za dhahabu, jambo litakaloongeza hamasa na ushindani katika tukio hilo kubwa la kitaifa.
Akhwar alisema,Bunge Marathon ya mwaka huu inaendeshwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya riadha, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza michezo na kuhamasisha afya kwa jamii.
Xxx

