Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kuimarisha vitengo vya tathmini na ufuatiliaji katika kila wizara ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Akijibu swali la Mbunge wa Monduli, Isack Copriano, aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuimarisha timu hizi ili kuharakisha majibu kwa wananchi na kero zao, Dkt. Nchemba alisema vitengo hivyo vitapewa rasilimali za kutosha.
“Kwenye kila wizara, kuna hivi vitengo vya ufuatiliaji na tathmini. Tunapanga kuongeza bajeti zao ili viweze kutimiza wajibu wao katika ufuatiliaji wa miradi na shughuli zote za Serikali,” alisema.
Dkt. Nchemba pia alibainisha hatua nyingine za kuimarisha mawasiliano na wananchi, ikiwemo kuanzishwa kwa kituo cha kupokea simu (Call Centre) namba 190, ambacho kinawapa wananchi nafasi ya kutoa kero zao na kupata majibu moja kwa moja.
Aidha, Waziri Mkuu alisema Serikali inalenga kurejesha utaratibu wa kila kiongozi kubeba hoja za wananchi kupitia rejesta maalumu, zitakazotumika katika ofisi za viongozi kurekodi kero na kutoa mrejesho serikalini kila mwisho wa mwezi.
“Utaratibu wa kupokea kero siyo wa kwenye ziara tu. Kila mwezi viongozi watapaswa kutoa taarifa ya idadi ya wananchi waliowahudumia, majibu waliyoyatoa, namba za simu za wananchi waliowahudumia na jinsi hoja hizo zilivyotatuliwa,” alisisitiza.
Dkt. Nchemba aliongeza kuwa, lengo ni kuhakikisha wananchi hawatahitaji kwenda kutafuta majibu kwa viongozi, bali hoja zao zinashughulikiwa ipasavyo na kuripotiwa kwa ufanisi.

