Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, amesisitiza umuhimu wa kudumisha mshikamano, weledi na uwajibikaji katika sekta ya maji nchini.
Amesema juhudi za pamoja zinapaswa kuendelezwa ili kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi wote kwa ufanisi zaidi.
Mwajuma ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kutambuliwa na wafanyakazi wanawake wa sekta ya maji, waliomkabidhi tuzo maalum kwa kuthamini mchango wake mkubwa katika kuimarisha na kuendeleza sekta hiyo nchini.

Aidha, aliwashukuru wanawake hao kwa heshima waliompatia.
Katibu Mkuu huyo pia amewahi kuibuka kinara kama Mhandisi Mama Bora nchini Tanzania, jambo linalodhihirisha umahiri wake katika taaluma na uongozi.
Hafla hiyo fupi imefanyika katika Ofisi za Bonde la Wami-Ruvu mkoani Morogoro, sambamba na tathmini ya maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani sekta ambayo inawagusa kwa kiasi kikubwa wanawake nchini.

Akikabidhi tuzo hiyo kwa niaba ya wafanyakazi wanawake wa sekta ya maji, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Nyasa, Elice Engelbert, amesema hatua hiyo inalenga kutambua uongozi thabiti wa Katibu Mkuu Mwajuma pamoja na mchango wake katika kusimamia utendaji kazi wenye tija,
Unaozingatia usawa wa kijinsia na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

