Na Mwandishi Wetu
WATAALAMU wa uhifadhi wa wanyamapori wamesema tembo wana mchango mkubwa katika kusaidia kuotesha na kusambaza mimea yenye mbegu ngumu kama ukwaju na ubuyu kutokana na mfumo wao wa mmeng’enyo wa chakula.
Hayo yalielezwa na mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Revocatus Meney, wakati wa kongamano la maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani lililofanyika Machi 3, mwaka huu 2026.
Meney alifafanua kuwa tembo wana utumbo mrefu unaofikia takribani mita 14, ambao husaidia kulainisha maganda ya mbegu ngumu wanazokula kupitia matunda.
Baada ya kupita katika mfumo wao wa mmeng’enyo wa chakula, mbegu hutolewa nje pamoja na kinyesi.
Mchakato huo hulainisha au wakati mwingine kupasua maganda ya mbegu, jambo linalorahisisha mbegu kuota.
Kwa mujibu wa wataalamu wa ikolojia, hali hiyo ni sehemu ya mchakato unaojulikana kama uenezaji wa mbegu kupitia wanyama wanaokula matunda.
Wanyama husambaza mbegu katika maeneo mbalimbali wanapopita, hivyo kusaidia kueneza mimea katika mazingira tofauti.
Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa tembo ni miongoni mwa wanyama wanaochangia katika kusambaza mbegu za miti katika mifumo ya ikolojia ya savana na misitu ya tropiki.
Utafiti uliochapishwa katika jarida la Biological Journal of the Linnean Society umebaini kuwa mbegu za baadhi ya miti kama Balanites maughamii zina uwezekano mkubwa wa kuota baada ya kupita katika mfumo wa mmeng’enyo wa tembo.
Utafiti huo ulionyesha kuwa kiwango cha uotaji wa mbegu kiliongezeka kutoka asilimia 11 hadi asilimia 74 baada ya kupita tumboni mwa tembo.
Pia imeelezwa kuwa tembo wanaweza kusambaza mbegu kwa umbali wa kilomita kadhaa kutoka walikokula matunda.
Kwa upande mwingine, Meney alisema Tanzania imepiga hatua katika uhifadhi wa tembo.
Takwimu za serikali zinaonyesha idadi ya tembo imeongezeka kutoka 43,330 mwaka 2014 hadi zaidi ya 60,000 katika miaka ya karibuni kutokana na juhudi za kupambana na ujangili na kuimarisha ulinzi wa hifadhi.
Hata hivyo, changamoto ya sasa ni kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na tembo kutokana na kupanuka kwa shughuli za kibinadamu katika maeneo ya wanyamapori.
Aidha, mhadhiri kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika – Mweka, Dkt. Never Mwambela, alisema matumizi ya mimea dawa yanatokana na tafiti za kisayansi na yanaweza kusaidia matibabu ya magonjwa pamoja na kukuza uchumi kupitia biashara ya bidhaa za asili.

