Walimu Walalamikia Changamoto za Maslahi
Na Lucy Ngowi
DODOMA: CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimeiomba Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, kurekebisha sheria, kanuni na kuweka miongozo itakayohakikisha uendeshaji wa vyama vya wafanyakazi unakuwa katika mazingira ya usawa na ushindani wa haki unaozingatia utoaji wa huduma bora.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa CWT, Joseph Misalaba, mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, katika Kikao cha Baraza la Taifa la CWT kilichofanyika jijini Dodoma.

Misalaba amesema utekelezaji wa shughuli za vyama vya wafanyakazi nchini umekuwa ukikabiliwa na changamoto zinazotokana na mkanganyiko wa sheria, kanuni na miongozo, hali inayosababisha mazingira yasiyo sawa.
Ametolea mfano uhuru wa upangaji wa ada za wanachama, uliosababisha tofauti kubwa za ada kati ya chama kimoja na kingine.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria, chama chenye wanachama wengi hubeba majukumu ya kuwawakilisha watumishi wote wa kada husika, hivyo kubeba gharama kubwa za uendeshaji, ajira, utetezi na majukumu mengine ya kisheria.

Hali hiyo ni tofauti na vyama visivyo na wajibu huo, jambo linaloviwezesha kutoza ada ndogo na kuwachanganya watumishi kuchagua vyama kwa misingi ya makato nafuu badala ya huduma.
Pia ameeleza changamoto ya ushughulikiaji wa madeni yasiyo ya mishahara kwa walimu, ambayo hutofautiana kati ya halmashauri, na kusababisha kukosekana kwa usawa.
Ameashauri kurejeshwa kwa kamati za uhakiki na madeni hayo kubebwa na serikali kuu.
Aidha, Misalaba amesema walimu wanaojiendeleza kielimu hawatambuliwi ipasavyo wanaporejea kazini, hali inayowakatisha tamaa.
Ameomba serikali kutafakari upya ili walimu wanaoongeza ujuzi watambuliwe na kupandishwa vyeo stahiki.

Kwa upande wake, Waziri Deus Sangu amesema serikali imeimarisha majadiliano na CWT, ambapo mwaka 2024/2025 vikao 23 vya ndani na kimoja cha kitaifa vilifanyika.
Ameongeza kuwa walimu 415,719 wamepandishwa madaraja na walimu 110,038 wamelipwa madeni ya mishahara yenye thamani ya takribani Sh Bilioni 125.16, hatua inayoonesha dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu.

