Na Lucy Ngowi
DODOMA: RAIS wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Dkt. Suleiman Ikomba amesema walimu nchini wamekuwa wakiachwa pembeni bila kulipwa stahiki za masaa ya ziada ya kazi pamoja na posho ya ufundishaji, hali ambayo si sawa.
Dkt. Ikomba ametoa kauli hiyo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, katika kikao cha Baraza la Taifa la Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kilichofanyika jijini Dodoma.
Amesema suala la Posho ya ufundishaji limeainishwa wazi katika Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009, kifungu (L)2 kifungu kidogo cha 21, kinachotamka kuwa stahiki za malipo ya masaa ya ziada ya kazi ni halali kisheria kwa watumishi wa umma, wakiwemo walimu, ingawa kwa vitendo hazitekelezwi.

Ameeleza kuwa walimu wanahudumiwa na vyombo visivyopungua vitano vinavyohusika na uamuzi na utekelezaji, hali inayosababisha vyombo hivyo kukwamishana.
Amesema hali hiyo imekuwa kikwazo katika kufikiwa kwa maono na maslahi ya walimu na inahitaji kuangaliwa upya.
Pia Dkt. Ikomba amesema kitaaluma na kimaadili, mwalimu anatakiwa kuwahi kufika shuleni kabla ya wanafunzi.

Ameeleza kuwa walimu hufika shuleni saa 12 asubuhi ili kuwapokea wanafunzi na mara nyingi huondoka saa 10 au 10:30 jioni.
“Hata hivyo, licha ya kufanya kazi zaidi ya saa rasmi, walimu hawapati malipo ya saa za ziada wala Posho ya ufundishaji, jambo ambalo haliko sawa,” amesema.
Aidha, amesema suala la
malimbikizo ya madai ya malipo na upandishwaji wa vyeo limeanza kupoteza mwelekeo.

Amebainisha kuwa awali kulikuwa na utaratibu mzuri wa kupandisha vyeo mwezi Julai, lakini kwa sasa walimu hupandishwa katika miezi tofauti kama Julai, Agosti au Septemba bila mpangilio unaoeleweka.
Ameshauri kuwa utaratibu huo wa awali uzingatiwe.
Kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, kifungu cha 13 kikisomwa pamoja na Kanuni za mwaka 2009 kifungu (L)2, Dkt. Ikomba amesema baadhi ya malipo ya likizo na posho ya kujikimu yamekuwa yakisahaulika na yanapaswa kulipwa kwa wakati.
Vilevile, amesisitiza kurejeshwa kwa vyombo halali vya kisheria kwa ajili ya majadiliano, ili walimu washirikishwe kikamilifu katika maamuzi yanayohusu utekelezaji wa masuala yao.

Amesema walimu ni kioo cha jamii na nguzo ya taifa kupitia elimu, hivyo anayestahili heshima apewe heshima.
Katika hatua nyingine, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua Waziri anayesimamia Wizara ya Vyama vya Wafanyakazi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema uimara wa CWT ni uimara wa sekta ya elimu Tanzania.
Amesema jumla ya walimu 415,719 wamepandishwa madaraja na walimu 110,038 wamelipwa madeni ya mishahara yenye thamani ya Sh. Bilioni 125.16, hatua inayothibitisha dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha maslahi ya walimu nchini.


