Na Lucy Lyatuu, Dodoma
SERIKALI imewataka watumishi wa umma wapya waliopata ajira kwa mwaka 2026 na kupangiwa vituo vyao vya kazi kutambua kuwa kwa sasa hakutokuwa na mabadiliko ya vituo vyao vya kazi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete, amesema hayo jijini hapa wakati akielezea utekelezaji wa maelekwzo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha siku 100 tangu alipoingia madarakani.
Kikwete amesema kwa sasa Serikali haitafanya mabadiliko ya vituo vya kazi kwa watumishi wa umma kwa kuwa mpangilio wa nafasi hizo ni kwa mujibu wa mgawango wa eneo husika.
Amesema na kwa watumishi ambao hawataripoti katika vituo vyao vya kazi ndani ya siku 14 tangu kupata barua nafasi zao zinaweza kuchukuliwa na wengine ambao walibakia katika kanzidata.
Kikwete amewataka waajiri pia wanapowapokea watumishi hao kutoa taarifa zao kwa Mhariri mkuu wa gazeti la serikali ili kutambuliwa.
” Yapo maombi mengi kutoka kwa watumishi wakiomna nafasibalimbali za kazi lakinibpia yapo maombi ya kubadilishwa vituo vya kazi, maombi hayo hayawezi kufanyiwa kazi kwa sasa, ” amesema Waziri Kikwete
Amebainisha kuwa nafasi zote za kazi zilitolewa kwa kuzingatia uhitaji wa kila Halmashauri au mwajiri husika, hivyo kufanya mabadiliko ya vituo vya kazi kungepunguza idadi ya watumishi waliopangwa katika maeneo husika na kuathiri mgawanyiko uliopangwa na Serikali.
Aliongeza kuwa katika siku 100 tangu Rais Dkt Samia kuingia madarakani tayari watumishi wapya 12,000 wamepata ajira wakiwemo wa kada ya afya 5000 na elimu 7000.
Kikwete amesema watumishi wapya 735 walioripoti katika vituo vyao vya kazi kabla ya kufungwa kwa mfumo wa mishahara tayari wamepewa mishahara kwa kuwa waliripoti kabla na kwamba watumishi wote wataingizwa kwenye mfumo wa mshahara kadri walivyoripoti katika vituo vyao.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 serikali ina mpango wa kutoa ajira nyingine 41,500 katika kada mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, kilimo, uvuvi, uhandisi, zimamoto na hata polisi na kuwaomba wananchi kuendelea kutumia mfumo wa kuomba ajira ili kipindi zikitangazwa waweze kuwa miongoni mwa watakaochukuliwa.
Katika hatua nyingine Kikwete amesema katika kipindi cha siku 100,Wizara eanzisha mfumo wa uwajibikaji ili viongozi wa umma kuzungumza na wananchi moja kwa moja ili kujibu maswali na malalamiko yao.
” Mfumo huu ni rafiki “Sema na Kiongozi”ni Mfumo wa kielekteoniki umeundwa kupokea malalamiko lengo likiwa ni kuimarisha utawala bora na viongozi wanaohusika wanaanzia ngazi ya wilaya na mkoa na kwamba wananchi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao na sauti zao kusikilizwa na kutolewa maamuzi, ” Amesema.

