Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WANAFUNZI wapya na wanaoendelea wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) wametakiwa kuwajibika katika masomo, kuwa na nidhamu ili kuhitimu kwa wakati.
Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Alex Makulilo, amesema hayo katika hotuba yake ya ukaribisho kwa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
Amesema wanafunzi wanapaswa kuwa makini na masomo yao na kufuatilia programu za ufundishaji, hususan mihadhara ya mtandaoni kupitia programu tumizi ya Zoom.

“Napenda kuwakumbusha kwamba kusoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kunahitaji nidhamu binafsi na kujituma,” amesema Profesa Makulilo.
Aidha, amesema chuo kitaendelea kutoa ratiba za ufundishaji mara kwa mara ili wanafunzi wafuatilie masomo bila kuachwa nyuma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Mkoa cha OUT – Dodoma, Dkt. Mohamed Msoroka, amesema kusoma kwa mafanikio kunawezekana kwa kila mtu, hasa kwa wale wanaojituma na kutumia muda wao vizuri.

Amesisitiza wanafunzi kujihusisha kikamilifu katika vipindi na mihadhara ya mtandaoni pamoja na ile ya ana kwa ana, na kutafuta msaada wanapouhitaji.
Amesema kwa kuwa wadahiliwa wengi ni watu wazima wenye familia, ajira na majukumu mengine, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilianzishwa ili kuwapa urahisi, uhuru na fursa ya kuendelea na elimu ya juu bila kuathiri majukumu yao.
“Mafanikio katika ujifunzaji kwa njia ya elimu huria na ya masafa yanahitaji nidhamu binafsi, kujitolea na uwezo mzuri wa kusimamia muda,” amesema Dkt. Msoroka.
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Kituo cha Mkoa cha Dodoma, Sabina Mpigauzi, anayesomea ualimu, ametoa wito kwa watumishi wa umma na sekta binafsi kujiendeleza kitaaluma kupitia Chuo hicho kwani kinawawezesha kuendelea na masomo bila kuathiri majukumu yao mengine kama ajira, malezi na uangalizi wa familia.

